Siku hizi, katika kila watu kumi
wanaotumia mtandao, basi angalau watano kati ya hao wanatumia mitandao
jamii. Kuna baadhi ya watu wamegeuza mitandao hii kuwa kama ni sehemu ya
mawasiliano, ama ya mtu kwa mtu au ya kibiashara. Siku hizi, si kitu
cha kushangaza kusikia mtu maarufu au kiongozi fulani atakuwa kwenye
Facebook saa fulani kwa ajili ya kujibu maswali ya wananchi / mashabiki
wake. Mitandao hii ni kama vile Facebook, Twitter, Jamiiforums nk, hivyo
basi, hatuwezi kuepuka ushawishi wa mitandao jamii katika jamii yetu.
Matumizi bora ya mitandao jamii huweza kuleta faida nzuri sana, ila
huwa kinyume pale inapotumika sivyo, ama kwa kutokujua ama kwa kuamua.
Hivyo leo hii tuangalie mambo kadhaa ya kuepuka unapotumia mitandao
jamii.
1. Epuka kujiacha wazi kwenye mitandao jamii.
Kuna baadhi ya watu wamegeuza mitandao
jamii ni dunia yao nyingine kabisa, wao kila kitu wanachokifanya
utakiona kwenye mitandao jamii, kala nini, anadate na nani, kavaa nguo
gani nk. Mitandao jamii ni uigaji (Simulation)
ya maisha ya halisi.Tukiwa kwenye maisha halisi, sio watu wote
wanaoweza kujua maisha yako kwa undani,kwani kuna vikomo, kuanzia wale
mulio nyumba moja, munaofanya kazi pamoja nk.
Ingawa kwenye mitandao jamii wengi wanaweza kuchunga kwa kutumia michungo ya ufaragha (Privacy setting)
lakini si wote wanaojua hilo, pia tumeona mamia ya akaunti za watu
zikivamiwa na wavamizi wa mtandao (Hackers) na kuweka hadharani taarifa
zao nyingi.
Hivyo epuka kuweza kila kitu kwenye mitandao jamii, kula na kikomo na
pia anza kuchunga marafiki zako juu ya nani anaweza kuona nini. Unaweza
kuangalia Video HAPA jinsi ya kuchunga ufaragha kwenye Facebook.
2. Jichunge kwenye utumaji.
Je ushawahi kusikia mtaani wanasema jamaa ana gubu (anaongea sana?),
kwenye mitandao jamii pia kuna watu wana gubu, wanachonga sanasana. Hawa
ni wale watu ambao kila dakika wametuma kitu kipya, hii sio tu hufanya
kupoteza mvuto kwa wanaokufuatilia, bali pia umuhimu wa makala zako
hupungua. Binafsi huondoa watu aina hii kwenye mlisho wa maboresho (activities feeds) bila hata kujiuliza.
Hivyo, ili kuepuka kutengwa au kuonekana unachonga sana, chunga idadi ya maboresho unayotuma kwa siku.
3.Epuka kutuma makala za ngono, dini au siasa kama wewe si muhusika.
Hivi ni vitu ambavyo huathiri watu wengi sana, chukulia mfano wewe ni
rafiki wa bwana X, unafungua Facebook au Twitter yako unakutana na
picha ya ngono imejaa kwenye mlisho wa maboresho toka kwa rafiki yako.
Ukweli ni kuwa utajisikia vibaya mno ama kama na wewe ni wa aina hiyo.
Hii pia ni sawa na kwa mambo ya dini na siasa.
Nchi yetu ikiwa ni nchi isiyo na dini,
ila watu wake wamechanganyika mnomno, kwenye kila marafiki zako wawili,
kuna mmoja ni wa dini nyingine, hivyo epuka kutuma makala za dini
zinazoudhi, zenye kebehi au kuudhi wengine. Jaribu kuwa mtu ambaye
utaweza kuishi na watu wote. Mfano huu pia tuuchukue kule uraiani, kuna
baadhi ya watu hukimbiwa, hivyo chukua tahadhari kabla ya kukimbiwa.
4. Usihamishie hasira zako kwenye mitandao jamii.
Kuna baadhi ya watu, wakishauziwa nyumbani, hasira zinaishia kwnye
mitandao jamii,amini usiamini, mitandao jamii haiwezi kukusaidia
kutuliza hasira zako zaidi ya kukupotezea muda na kujidhalilisha. Ni
sawa na yule mtu mwenye ugomvi na mke / mume wake halafu anapita kila
nyumba kutangazia mapungufu ya mwenza wake, jamii nzima inajua, siku
mutakaporudiana, watu wote washajua mapungufu ya mwenza wako, je utafuta
toka kwenye vichwa vyao?
Kwenye mitandao jamii vilevile, kuna baadhi ya watu kuhifadhi kila
unachotuma na siku ya siku watatumia kuja kukashambulia. Kaa mbali na
mitandao jamii kama unaona hauwezi kuchunga mhemuko (emotion) wako.
5.Siyo kila mtu lazima awe rafiki yako.
Chukulia mfano mitaani tunamoishi, kuna watu wa aina mbalimbali, na
siyo kila mtu ni rafiki yako, kuna baadhi ya watu hata hautaki
kuwasogelea kutokana na tabia zao, hii ni sawa kwenye mitandao jamii.
Epuka kukubali maombi ya urafiki toka kwa kila mtu, haswaa ambao
hauwafahamu. Marafiki sio tu huweza kutumika kujenga taswiura yako, bali
kuna baadhi ya marafiki si marafiki, hivyo chunga marafiki zako la
sivyo ipo siku utakuja kujuta.

0 comments:
Post a Comment