Rais Jakaya Kikwete ametangaza kuanza mara moja mpango mkubwa wa
ujenzi wa kimataifa wa reli ya kati baada ya kupatikana kwa mafanikio
makubwa ya ujenzi wa miundo mbinu ya barabara kwa kiwango cha lami
nchini kote.
Mh rais kikwete ametangaza mpango huo mkubwa wa
ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa,wakati akihutubia
maelfu ya wananchi wa mji wa Old Maswa wilayani Bariadi mkoani Simiyu
muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa barabara ya
kilometa 71.7 inayojengwa na kampuni ya cc ya nchini China kwa kutumia
fedha za ndani kiasi cha shilingi bilioni 70.
Hata hivyo rais Kikwete,amesema serikali,imekuwa
ikitumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara yakiwemo
madaraja ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, huku akisema kati ya
madaraja makubwa matano yalipangwa kujengwa baada ya uhuru,rais wa
kwanza Mwl Julius Nyerere ameweza kujenga daraja la Kirumi mkoani Mara
na rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa amejenga daraja la mto Rufiji
na sasa serikali yake imekamilisha ujenzi wa madaraja matatu
yaliosalia.
Awali waziri wa ujenzi Mh. John Pombe
Magufuli, akimkaribisha rais Kikwete kuzungumza na wananchi ambao
wamejitokeza kushuhudia uwekaji wa jiwe hilo la msingi,amesema ujenzi wa
barabara hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa mkoa wa Simiyu
kwa kuunganishwa na mikoa ya Mwanza na mara pamoja na nchi jirani ya
Kenya,huku mtendaji mkuu wa wakala wa barabara mhandisi Patrick
Mfugale,akitoa kilio kwa rais kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya
kulipa wakandarasi nchini.
CHANZO:ITV

0 comments:
Post a Comment