Historia ya Tanzania kuwa na Katiba Mpya
itakayopatikana kutokana na maoni ya wananchi ilianza Desemba 31, 2011
wakati Rais Jakaya Kikwete akilihutubia taifa, alikiri wazi kuwa sasa
inahitajika Katiba Mpya ili kuendana na wakati wa sasa.
Baadaye Rais Kikwete aliwateua wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba na ilianza kazi
yake ya miezi 18, kuanzia Mei 3, mwaka 2012.
Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi nchi nzima na kuandaa rasimu ya kwanza ya Katiba ambayo iliitoa Juni 4, mwaka huu.
Baada ya kutolewa kwa rasimu hiyo wananchi
walipewa muda wa kuipitia na kuitolea maoni katika Mabaraza ya Katiba ya
wilaya, yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2, mwaka huu.
Maoni hayo yalikusanywa na tume hiyo kwa ajili ya
kuyachambua na kutoa rasimu ya pili ya Katiba ambayo inatarajiwa
kutolewa Desemba 30, mwaka huu.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitakiwa kumaliza
kazi ya kuandaa rasimu ya pili Desemba 15, mwaka huu, lakini Rais
Kikwete aliiongezea siku 14 zaidi na hivyo kuifanya iweze kuendelea na
kazi hadi Desemba 30.
Hatua hiyo ya Rais Kikwete kuiongezea muda tume
hiyo ilikuwa ya pili, kwani mara ya kwanza tume hiyo iliomba kuongezewa
muda wa siku 45, kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu.
Kabla ya kuomba kuongezewa muda mara ya kwanza, tume ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba 30.
Kwa uamuzi wake, wa kuiongezea Tume hiyo siku
nyingine 14, Rais Kikwete ameiongezea tume hiyo jumla ya siku 59 kati ya
60 ambazo anaruhusiwa kisheria.
Kifo cha Dk Sengondo Mvungi
Hatua ya Rais kuiongezea muda Tume ya Mabadiliko
ya Katiba ilitafsiriwa kama kutoa fursa kwa wajumbe wa tume hiyo
kujipanga upya baada ya kifo cha mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Dk
Sengondo Mvungi aliyefariki dunia Novemba 12, mwaka huu nchini Afrika
Kusini alikokuwa akitibiwa baada ya kujeruhiwa kwa mapanga na watu
wanaotuhumiwa kuwa majambazi, nyumbani kwake mkoani Dar es Salaam.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment