Home » » WAZIRI NYALANDU:ASKARI KUPEWA CHAO MAPEMA KABLA YA OPERESHENI AWAMU YA PILI

WAZIRI NYALANDU:ASKARI KUPEWA CHAO MAPEMA KABLA YA OPERESHENI AWAMU YA PILI

Written By kitulofm on Tuesday, 4 February 2014 | Tuesday, February 04, 2014


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema askari 2,000 waliounda kikosi maalumu cha Operesheni Tokomeza Ujangili watalipwa fedha zao kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya operesheni  hiyo.
 
Nyalandu alitoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, kusema kuna zaidi ya askari 2,000 waliounda kikosi maalumu kwa ajili ya operesheni hiyo ya awamu ya kwanza hawakulipwa posho zao hadi sasa.
 
Akizungumza na mabalozi wa nchi mbalimbali jijini Dar es Salaam jana wakati wa kikao cha kujadili njia shirikishi za kutumia katika vita ya ujangili, Nyalandu alisema watahakikisha wanalipa madeni yote ya askari hao kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo huku akisisitiza kwamba zoezi hilo ni endelevu na lilisitishwa ili kuondoa kasoro zilizojitokeza wakati wa operesheni hiyo awamu ya kwanza.
 
“Hili ni zoezi endelevu,  lilisitishwa kwa ajili ya kuibuka kwa kasoro kadhaa… askari wote walioshiriki katika operesheni hiyo watalipwa wakiwemo wale wa askari wanyamapori na wenzao wa Jeshi la Wananchi (JWTZ),  hatutaaanza awamu ya pili na madeni,” alisisitiza.
 
Kuhusu awamu ya pili ya operesheni hiyo itakayoanza muda wowote huku jumuiya ya kimataifa ikiungana katika vita dhidi ya ujangili, ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) litaongoza vita hiyo.
 
Kwa mujibu wa Nyalandu nchi mbalimbali zimekubali kuisaidia Tanzania katika mikakati ya muda mrefu na mfupi ya kupambana na ujangili.
 
Alizitaja baadhi ya nchi hizo ni Uingereza, Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Hispania, Japan na China huku akizitaja taasisi kubwa zilizotia mkono kuwa ni Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) na Umoja wa Mataifa (UN).
 
Alisema nchi hizo zitasaidia kujua nchi ambazo soko la meno ya tembo na faru lipo kwa ajili ya kuuzwa, ikiwemo askari wa kimataifa (Interpol).
 

Nyalandu alisema kuna uhaba wa askari wa wanyamapori 3,767 na kufafanua kuwa hivi sasa wapo askari 1,088 pekee na wanaohitajika ni askari 4,855.
CHANZO:TANZANIA DAIMA
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

KITULO FM LOGO

KITULO FM LOGO
Tusikilize masaa 18 kwa siku kupitia masafa ya 97.0 FM ukiwa wilayani Makete mkoani Njombe na maeneo ya jirani

WASOMAJI WETU

KUMBUKUMBU YA HABARI ZETU

 

Copyright © 2013. KITULOFM BLOG - Haki zote zimehifadhiwa
Imetengenezwa na Edwin Moshi
Inawezeshwa na Kitulo Fm