Vijana wakivusha mizigo ya wasafiri kutoka Rujewa kuelekea Madibira
wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Barabara hiyo imekatika kwa miezi miwili
sasa, baada ya kusombwa na maji.
Vijana wanavusha mizigo hiyo kwa
Sh.1,000-3,000 kwa kila mzigo huku wajawazito, watoto na wazee wakiwa
wanapata taabu kuvuka(Picha na Gordon Kalulunga).
Kulia ni kamanda wa UVCCM Wilaya ya
Mbarali mkoani Mbeya, Ibrahimu Ismail, akiwa na Mwenyekiti wa UVCCM
wilayani humo, katika eneo ambalo Barabara ya Rujewa na Ubaruku
imekatika.
Vijana wakivusha mizigo.
Kushoto ni kamanda wa UVCCM Wilaya ya Mbarali mkoani
Mbeya, Ibrahimu Ismail, akiwa anawasikiliza wakazi wa karibu na eneo hilo ambalo barabara imekatika.
Kijana Caros, akimweleza kamanda wa UVCCM Wilaya ya Mbarali mkoani
Mbeya, Ibrahimu Ismail, jinsi wanavyoshauri Barabara hiyo kujengwa lakini wanapuuzwa na wataalam(wasomi).
Wakati wengine wanalia, wengine kicheko kwa kuvua samaki aina ya dagaa.....
Na Gordon
Kalulunga, Mbarali
MVUA
zinazoendelea kunyesha nchini, zimesababisha kukatika mawasiliano ya Barabara
inayounganisha eneo la Rujewa na Madibila wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Wakizungumza
na Mwandishi wa habari aliyefika eneo lililoharibika vibaya, baadhi ya wananchi
waliokutwa eneo hilo wakivuka ndani ya maji hayo, walisema tangu mwezi Februari
mwaka huu eneo hilo halipitiki kwa gari aina yeyote.
Walisema eneo
hilo ambalo lipo bondeni, limekuwa korofi kutokana na ukaidi wa wasomi ambao
hawataki kusikiliza ushauri wa wenyeji wa maeneo hayo ili kuhamisha barabara
hiyo.
‘’Kila mwaka
tunawashauri kuwa Barabara hii inapaswa kuhamishiwa upande wa juu, lakini
wanakataa na kusema kuwa wakihamisha hawataweza kula pesa kila mwaka ambapo
Barabara hii inasombwa na maji’’ alisema mwananchi Caros Elias Mbala.
Mwenyekiti
wa UVCCM wilaya ya Mbarali, Amin Kimulungu akiwa sambamba na Kamanda wa UVCCM wilayani
humo, Ibrahimu Mwakabwanga, alisema hali ya kukatika mawasiliano ya barabara
hiyo imekuwa shida kubwa kwa wananchi wa Madibila, Rujewa na maeneo mengine
kila mwaka.
Alisema
kinachosikitisha kipande hicho cha barabara kilichosombwa na maji kinatengewa
fedha kila mwaka bila kupata ufumbuzi wa kudumu jambo ambalo linakiondolea
chama chake heshima ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa mwaka 2005-2010 na
2010-2015.
‘’Maji yote
haya yanatoka katika mto wa asili eneo la Ilembula na Malangali Mufindi
wilayani Iringa kisha kufurika katika wilaya hii ambayo inategemea maji haya
kwa ajili ya kilimo cha Mpunga’’ alisema Kimulungu.
Aliongeza
kuwa kuna wakati yeye mwenyewe aliwahi kuhusika kumkodia gari upande wa pili
mjamzito mmoja ambaye alizidiwa kutoka Madibila kwenda hospitali ya wilaya
Rujewa baada ya kukwama eneo hilo na kutokuwepo na gari ya kuelekea Rujewa.
Kutokana na
barabara hiyo kusombwa na maji, bei ya nauli imepanda kutoka Sh 5,000 mpaka
8,000 huku mizigo ikivushwa na vijana kwa Sh 1,000 mpaka 3,000 na shida kubwa
ikiwa kwa watoto, wazee na wajawazito ambao hulazimika kukunja nguo zao na
kujitosa kwenye maji ili kuvuka upande wa pili na kutafuta usafiri mwingine.
Barabara hiyo
inaelezwa kuwa na bajeti ya kiwango cha Lami lakini mpaka sasa utekelezaji wake
umebakia mikononi mwa wataalam huku wananchi wakibaki na sintofahamu ya
mawasliano ya barabra hiyo.
0 comments:
Post a Comment