Vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) vilivyopo kwenye vikosi vya Umoja wa Mataifa, vimeongeza kasi ya
kukabiliana na waasi wa Kundi la M23 na kufanikiwa kutwaa maeneo mengine
zaidi ikiwemo Milima ya Mbuzi iliyokuwa ikitumika kama maficho kwa
waasi hao.
Eneo la Milima ya Mbuzi lililoko karibu na mpaka
na Uganda ni moja ya ngome za mwisho za kundi hilo ambalo lilianza
kupoteza udhibiti wa maeneo muhimu tangu mwishoni mwa mwezi uliopita
wakati vikosi vya Congo kwa msaada wa vile vya Umoja wa Mataifa
vilipoanzisha operesheni maalumu ya msituni.
Kuzuka kwa mapigano hayo kumekuja wakati kukiwa na
taarifa zinazokinzana kutoka pande zote mbili kuhusiana na usalama wa
eneo hilo la Mashariki.
Wakati Vikosi vya Congo vikiwa vimetangaza
operesheni mpya iliyopewa jina la “Mkakati wa kufagia masalia ya waasi”,
naye kiongozi wa M23, Bertrand Bisimwa aliwataka askari wake kuweka
chini silaha ili kurejea kwenye meza ya mazungumzo nchini Uganda.
Duru za habari zinasema kuwa askari wa Congo
wakishirikiana na wale wa Umoja wa Mataifa wameendesha mashambulizi ya
angani na kufanikiwa kuwafurusha wanamgambo wa M23 walioweka kambi
maeneo ya Runyonyi na Chanzu umbali wa kilometa 80 Kaskazini mwa Mji wa
Goma. Imesemekana pia katika mapigano hayo raia sita walipoteza maisha.
Msemaji wa vikosi vya Umoja wa Mataifa Martin
Kobler alisema jana kuwa kitendo cha waasi wa M23 kuanzisha mashambulizi
kwa raia wakati walitangaza kuweka chini silaha ili kupisha mazungumzo
ya amani ni kitendo kisichokubalika.
Alisema kuwa mwenendo ulionyeshwa na M23
kutosimamia kauli zake, ndiyo sababu vikosi vya Umoja wa Mataifa
kuendesha mashambulizi ya angani na kuhaidi kufanya hivyo mpaka pale
waasi hao watapofurushwa kabisa katika ardhi ya Congo.
Hata hivyo kumekuwa na utata kuhusiana kuuawa kwa
raia sita ambao miili yao ilikutwa jana kwenye eneo la Bunagana lililoko
mpakani na Uganda.
Akizungumza na shirika la habari la AFP, Gavana wa
jimbo la Kivu Kaskanizi Julien Paluku hakuwa tayari kutaja upande
uliosababisha mauaji hayo.
Afisa wa Jeshi la Uganda, Luteni Kanali Paddy
Ankunda alisema mapigano hayo yalisababisha pia uharibifu katika maeneo
ya Uganda lakini hakuna raia yoyote aliyejeruhiwa.
Hivyo baadhi ya ripoti zinasema tangu kuanzishwa
kwa operesheni ya awamu ya pili zaidi ya raia tano wa Uganda
wamejeruhiwa. Kumekuwa na taarifa kuwepo kwa hali ya shamra shamra
kutoka kwa askari wa Congo walioingia katika Milima ya Mbuzi.
0 comments:
Post a Comment