Nembo ya Taifa ya Tanganyika (1961 – 1964) inatofautiana kidogo na nembo ya Tanzania
kwa kuwa, baada ya Muungano, iliongezewa bendera ya Tanzania na alama ya jembe na
shoka
Nembo ya Taifa inaonesha mwanaume na mwanamke wakiwa wameshikilia ngao iliyo kati
ya pembe za ndovu zilizosimama juu ya Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu kuliko yote
Afrika.
Pembe za ndovu zinaashiria utajiri wa wanyamapori na hifadhi za Taifa.
Robo ya juu inaonesha Mwenge wa Uhuru ambao ni ishara ya kuwapa matumaini waliokata
tama, heshima palipo na dharau na upendo palipo na chuki.
Sehemu ya juu ya nembo ina rangi ya dhahabu ikiwa ishara ya madini na chini yake
kuna bendera ya Tanzania. Rangi nyekundu chini ya bendera ya Taifa ni ishara ya udongo
na kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa. Sehemu ya chini ya nembo kuna
mistari ya pundamilia iliyowakilisha mawimbi ya bahari na maziwa kwenye mipaka ya
nchi pamoja na bahari inayozunguka Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano.
Juu ya alama hizi kuna mkuki, jembe na shoka kama ishara ya ulinzi na ujenzi wa
Taifa. Mwanamke na Mwanaume katika nembo hii ni ishara ya usawa wa jinsi na wamesimama
juu ya mimea ya pamba na karafuu, mazao makuu ya biashara kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Uhuru na Umoja” yameandikwa kwenye ukanda chini kabisa ya nembo, ambao ni wito maalum
wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment