Home » » SILAHA AZUIWA KUHUTUBIA KIGOMA NA WANACHAMA

SILAHA AZUIWA KUHUTUBIA KIGOMA NA WANACHAMA

Written By kitulofm on Monday, 9 December 2013 | Monday, December 09, 2013

Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mjini hapa wamefanya maandamano ya amani hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, kuomba kibali cha kumzuia Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa, asihutubie mkutano wa hadhara.
 
Maandamano hayo yaliyoongozwa na wapanda pikipiki (boda boda), yalianzia kijiji cha Mwandiga na kuishia Mwanza Stendi eneo la Manispaa ya Kigoma Ujiji.
 
Wanachama hao walidai wamefanya maandamano ya amani ya kumtaka Zitto Kabwe na siyo chama.
 
Wakizungumza na NIPASHE Jumapili,  walisema hawamtaki Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk.  Slaa Kigoma Ujiji na kumuomba Mkuu wa Mkoa  na Kamanda wa Polisi wa Mkoa kutotoa kibali cha kumruhusu kuhutubia mkutano kwa madai kuwa walimvua uongozi Zitto.
 
Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alivuliwa nyadhifa mbalimbali alizokuwa nazo ndani ya chama hicho, pamoja na wenzake wawili ambao ni mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitilla Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha aliyesimamishwa uongozi, Samson Mwigamba.
 
Wakati wa maandamano hayo, wanachama hao walisema kuwa viongozi wa ngazi  za taifa wamekuwa wakiwahujumu viongozi wa ngazi za chini wanaotokea mkoani Kigoma na kuwataja baadhi waliohujumiwa kuwa ni David Kafulila ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kusini na Amani Kabourou ambao wanachama hao walidai kuwa walitolewa kwa njama hivyo kwa sasa hawatakubali yaliyomtokea Zitto.
 
Aidha kutokana na sababu hizo, wanachama hao walisema kuwa wanamtaka Zitto kwanza, chama baadaye.
 
Mwenyekiti wa Chadema mkoani humo, Jafar Kasisiko, alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana na maandamano hayo alisema alipigiwa simu na Mwenyekiti Chadema wa Kigoma Kaskazini, Ali Kisara,  aliyemjulisha kuhusu maandamano hayo.
 
“Kisara alinieleza kuwa kesho (jana)  tutafanya maandamano ya amani mimi sikukubaliana nao kwa kuwa makao makuu walishaamua Dk. Slaa kufanya ziara hapa Kigoma, nilimweleza kuwa nipo na Slaa,” alisema.
 
Aidha, alisema  wanachama hao wameamua kufanya maandamao hayo bila uongozi wa mkoa wa chama hicho kujulishwa.
 
Kaimu Kamanda wa Polisi Kigoma, Zedekia Makunja  alipoulizwa kuhusiana na maandamano hayo, alisema yalikuwa na kibali kwa sababu wanachama waliomba kuyafanya lengo likiwa ni kutoa hisia zao.
 
“Sisi kama Polisi wa mkoa huu, Dk. Slaa akifika manispaa ya Kigoma Ujiji tutampa ulinzi kwani nia yetu hatutaki kutokee uvunjifu wa amani hapa,” alisisitiza.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

KITULO FM LOGO

KITULO FM LOGO
Tusikilize masaa 18 kwa siku kupitia masafa ya 97.0 FM ukiwa wilayani Makete mkoani Njombe na maeneo ya jirani

WASOMAJI WETU

KUMBUKUMBU YA HABARI ZETU

 

Copyright © 2013. KITULOFM BLOG - Haki zote zimehifadhiwa
Imetengenezwa na Edwin Moshi
Inawezeshwa na Kitulo Fm