Na Khamisuu Abdallah
HUKU mataifa duniani yakiendelea na siku 16 za kupinga udhalilishaji wa
kijinsia, mambo yamegeuka Zanzibar ambapo wanawake wanadaiwa
kuwanyanyasa wanaume.
Kwa ilivyozoeleka wanawake ndio waathirika wakubwa wanaokabiliwa na
vitendo vya udhalilishaji, lakini hapa Zanzibar kibao kimewageukia
wanaume ambao kwa mujibu wa jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi zipo
kesi kadhaa zilizoripotiwa.
Akizungumza na Mwandishi wa gazeti hili huko Ofisini kwake Muembemadema,
Mkuu wa Dawati hilo Staff Sagenti Zahor Faki, alisema kumekuwa na
ongezeko kubwa la idadi ya wanawake wenye tabia ya kuwanyanyasa waume
zao ikiwemo kuwapa vipigo.
Alisema dawati lake limepokea kesi tisa za wanawake kuwadhalilisha
wanaume na kwamba kesi hizo zimeripotiwa kuanzia mwezi Januari mwaka huu
hadi Oktoba.
Alisema wanawake wengi wenye kufanya vitendo vya udhalilishaji hasa vya
kuwapiga waume zao, hufanya kwa kuvizia hasa wakiwa wanaume hao
wamelala.
Mkuu huyo alisema sababu kubwa zinazopelekea waume hao kupigwa na wake
zao zinatokana na wanawake wengi kuwa na wivu wa kupindukia katika ndoa
zao pamoja na migogoro ya kugombani mali.
Aidha akizitaja sababu nyengine alisema zinatokana na watoto wakati
wazazi wao wanapoachana huku mwanamke akizuia hati ya nyumba ambayo si
haki yake bila kukaa kulitatua tatizo hilo.
"Sababu hii inatokana na mume alieachana na mke wakati wakiwa wameshazaa
mwanamke huanza vurugu na kuzuia hati ya nyumba wakati si haki yake na
husema hatoi mpaka apewe kitu fulani bila ya kukaa pamoja na kulitatua
tatizo hilo", alifafanua Mkuu huyo.
Alifahamisha kuwa wanawake wengi wamekuwa wakiwavizia waume zao wakati
wakiwa usingizini na kuwajeruhi sehemu mbalimbali za miili ikiwemo
sehemu ya siri huku wakiwapa maneno makali.
Zahor alifahamisha kuwa mbali na malalamiko hayo lakini wanaume wengi
wamekuwa hawaripoti katika Dawati hilo kutokana na mambo ya aibu jambo
ambalo linawakosesha haki zao za msingi kama vile wanawake.
Hata hivyo Mkuu Zahor alisema hakuna hata lalamiko moja lililofikishwa
mahakamani bali mengine huyatolea uamuzi na mengine bado yanaendelea na
upelelezi.
Akizitaja changamoto zinazowakabili ni pamoja na wanawake wanaofanya
vitendo hivyo kuja na hukumu zao mikononi jambo ambalo ni kinyume na
sheria za nchi.
Hivyo aliwataka wanandoa kujua wajibu wao kwani ndoa ni hidaya huku
akiwasisitiza kuacha tabia ya kuishi kwa chuki na kusikiliza fitna za
watu ambao hawawatakii mema.
Pia aliwashauri wanaume hao kutoona tabu kufika katika vituo
vinavyohusika ili viweze kuwatetea kama wananawake ambao hupaza sauti
zao na kusikika haraka kutokana na kuundwa kwa tasisi mbalimbali kama
vile Zafela, Tamwa na Dawati la kijinsia.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maimam Zanzibar,
Sheikh Khamis Yussuf Khamis akizungumzia saula hilo alisema ni kweli
malalamiko hayo huwa yanaenda katika jumuiya yao.
Aidha alifahamisha kuwa jumuiya yao kesi hizo zinapotokezea huwa
wanasuluhisha kwa kutumia njia za kidini hasa kuwapa wanandoa elimu ya
kujua wajibu wao.
Hivyo aliwataka wanandoa hao kupata elimu ya kutosha kabla hawajafunga
ndoa ili kuondokana na matatizo mbalimbali ya hapa na pale.
Sambamba na hayo aliwashauri vijana wa kiume kufuata mawazo ya busara
kutoka kwa wazazi wao na sio kufuata utashi wa marafiki ambao
hawawatakii mema katika ndoa zao.
CHANZO:SWAHILIVILLA
0 comments:
Post a Comment