SERIKALI ya Uganda tayari
imeshaanza kulipa deni lake kwa Tanzania la dola za Marekani milioni 9.6
kati ya dola za Marekani milioni 18.4 ikiwa ni fidia kwa Tanzania kwa
mchango wake katika kumuondoa Idd Amin Dada Uganda mwaka 1978.
Hayo yalibainishwa bungeni jana na
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Shamsi Vuai Nahodha,
wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mbinga, John Komba (CCM).
Katika swali lake Komba alitaka kujua
kama Tanzania ilishaanza kudai fidia kwa Serikali ya Uganda kutokana na
mchango wake wa kuisaidia nchi hiyo kumuondoa Idd Amin na kumfanya Rais
wa sasa Yoweri Museveni kutawala kwa amani nchini humo.
Akijibu swali hilo, Nahodha alikiri kuwa
Tanzania ilipigana vita na Uganda kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 1979
kutokana na uvamizi uliofanywa na Uganda chini ya utawala wa Idd Amin
aliyevamia na kukalia sehemu ya ardhi ya Tanzania mkoani Kagera.
“Kwa kuwa vita hivyo vilitokana na
uvamizi wa Idd Amin, baada ya vita kumalizika Serikali ya Tanzania
iliitaka Uganda kulipa fidia. Serikali hiyo nayo ilikubali kuilipa
Tanzania fidia hiyo,” alisema Nahodha.
Alisema kwa bahati mbaya Serikali ya
Uganda haikutekeleza makubaliano hayo yaliyofanyika mwaka 1979 hivyo
Serikali ya awamu ya tatu ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mstaafuma
William Benjamin Mkapa ilifanya majadiliano tena na Uganda.
Alisema kutokana na majadiliano hayo
Serikali ya Uganda ilitakiwa kulipa fidia dola za Marekani milioni 18.4
na hadi sasa Serikali hiyo imeshalipa dola za Marekani milioni 9.6 fedha
ambazo ziliwekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali na nchi hiyo kubakiwa na
deni la dola za Marekani milioni 8.8.
Nahodha alisema majadiliano baina ya
Tanzania na Uganda yanaendelea ili sehemu ya fidia iliyobaki iweze
kulipwa chini ya Wizara ya Fedha ambayo ndio inayofuatilia deni hilo.
Akijibu swali la nyongeza la Komba la
kuitaka Tanzania imkumbushe Museveni juu ya namna Tanzania ilivyosaidia
nchi yake hivyo aache kuihujumu kwa kusaidiana na Rais wa Rwanda Paul
Kagame, Nahodha alisema siku zote Tanzania haimsaidii mtu ili kupata
shukurani. “
Tanzania ni nchi ya kipekee sana,
imebahatika kupata viongozi wenye sifa kubwa duniani kama Nyerere
(Mwalimu Julius), kiongozi huyu aliwahi kusema Waafrika ni ndugu na
Afrika yetu sote, tuliwasaidia Uganda kwa utu hatutegemei zaidi,”
alisisitiza.
Alisema hata juzi baada ya kifo cha Rais
wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Tanzania ilitoa tamko la
kumuenzi kwa kusisitiza uvumilivu, jambo ambalo limeipatia sifa kubwa
Tanzania. “Naomba tuendelee kuitunza sifa hii na si vinginevyo.”
CHANZO:HABARI LEO
CHANZO:HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment