Baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Makete likiendelea.
Diwani wa kata ya Matamba mh. Asheli Mwalyoyo akichangia hoja
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Mh. Daniel Okoka akiongoza kikao hicho
Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akitoa ufafanuzi kuhusu suala la leseni katika baraza hilo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete ambaye pia ni katibu wa kikao hicho Bw. Iddi Nganya akisoma taarifa ya rasimu ya bajeti ya halmashauri yake kwa mwaka 2014/2015.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula akisikiliza kwa makini hoja za madiwani katika kikao hicho.
Baraza maalum la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Makete mkoaniNjombe leo Januari 28 limejadili na kupitisha rasimu ya bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka 2014/2015
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Makete madiwani hao wamejadili hoja mbalimbali zilizopo katika rasimu hiyo ikiwemo uboreshaji wa namna ya kuongeza mapato kutoka kwenye vyanzo vyote vilivyoainishwa na halmashauri hiyo
Baadhi ya hoja zilizochangiwa na madiwani hao ni pamoja na halmashauri kuwa na vyanzo vya kukusanya mapato lakini kumekuwa na tatizo la mapato hayo kutofika kama yalivyokusanywa wakimaanisha kumekuwepo na kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya watendaji wanaokusanya mapato hayo
Diwani wa kata ya Matamba (CCM) Mh. Asheri Mwalyoyo ametolea mfano katika kata yake kuwa kumekuwepo na ukusanyaji wa mapato lakini taarifa zinazofika wilayani zinaonesha yamekusanywa mapato kidogo ilihali ana uhakika yamekusanywa mengi
"Tuchukulie kwenye kata yangu ya Matamba ushuru tu wa pombe kwa vilabu 10 tu ni shilingi 60,000/- kwa mwezi lakini kwenye taarifa huku wilayani inaonesha ushuru wa pombe za kienyeji ni 70,000/- sasa hii inashangaza maana tuna vilabu vingi, hapa ni kukosekana kwa uadilifu wa baadhi ya watendaji wanaokusanya mapato hayo" alisema Mwalyoyo
Naye diwani wa kata ya Tandala Mh. Egnatio Mtawa ameshangazwa na hatua ya rasimu hiyo kuonesha kutegemea kwa kiasi kikubwa mapato ya pombe na kudai kuwa wahusika wote wakiwemo watendaji na wao kama madiwani walikuwa wavivu wa kufikiri kubuni vyanzo vipya vya kukusanya mapato badala ya kutegemea ushuru wa pombe kwa kiasi kikubwa
Amesema hii inaashiria wananchi wazidi kunywa pombe kwa wingi ili mapato yapatikane lakini pia njia hiyo itachochea vilabu na baa kufunguliwa mapema tofauti na sheria inavyoruhusu hivyo kupata wingi wa wananchi watakao kuwa wamelewa muda wote hasa muda wa kufanya kazi
Aidha rasimu hiyo pia imeainisha vyanzo vipya vitakavyosaidia kuongeza mapato ya halmashauri ikiwemo ushuru wa majengo ambapo watu waliokwisha jenga nyumba tayari watakuwa wanalipia ushuru wa jengo kwa mwaka na wale ambao bado wana mpango wa kujenga watalipia kabla ya ujenzi kuanza
Halmashauri ya wilaya ya Makete ni miongoni mwa wilaya ambayo ina vyanzo vichache vya mapato hali inayosababisha upatikanaji wa mapato yake kuwa mdogo, hivyo inaendelea kubuni vyanzo vipya ili mapato yake yaweze kuongezeka zaidi ya sasa
0 comments:
Post a Comment