MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi imemhukumu kifungo
cha maisha jela mkazi wa Kijiji cha Mwese, Leonald William (19), baada ya
kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka
saba ambaye jina lake limehifadhiwa.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Chiganga Ntengwa, baada ya mahakama
kumtia hatiani kwa kosa hilo.
Katika kesi hiyo ambayo ilikuwa na washitakiwa wawili, mshitakiwa
mwingine, Ezekia Yohane, mwenye umri wa miaka kumi na saba
alihukumiwa adhabu ya viboko vinne kutokana na umri wake kuwa mdogo.
Washitakiwa hao walidaiwa kutenda kosa la kumlawiti mtoto huyo Julai
31, mwaka huu, majira ya saa mbili usiku nyumbani kwao mtoto huyo, ambapo
washitakiwa hao walikuwa wameajiriwa kufanya kazi ya kuchunga mifugo ya
baba mzazi wa mtoto huyo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Chiganga alisema baada ya kusikiliza
mwenendo mzima wa kesi mahakama imewaona washitakiwa wana
hatia.
Washitakiwa kabla ya kusomewa hukumu walipewa nafasi ya kujitetea
ambapo waliiomba Mahakama iwaachie huru kutokana na
kile walichodai kuwa walisingiziwa kosa hilo na baba wa mtoto huyo kwa kuwa
walikuwa wakimdai pesa za mishahara za muda mrefu.
Baada ya maombi hayo, Mwendesha Mashitaka Mkaguzi Msaidizi
wa Polisi, Ally Mbwijo, alipinga vikali maombi hayo na
kuiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa.
CHANZO:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment