IMEBAINIKA wanaume wengi wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na wake zao wanashindwa kuweka wazi vitendo hivyo kwa kuona aibu.
Hayo yalibainishwa juzi na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Moshi, Aisha Nyerere, kwenye uzinduzi wa Siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia Kanda ya Kaskazini.
Alisema licha ya kuwa vitendo vya ukatili vimekuwa zaidi kwa wanawake
na watoto lakini nao wanaume kwa sasa wanakabiliwa na vitendo hivyo.
“Naomba siku 16 za kupinga ukatili zitumike ipasavyo na hususan watu
wote wanaohudhuria kampeni hizi kama unaona kuna mwanamume jirani yako
anafanyiwa vitendo vya ukatili unaweza kumsaidia au mtu mwingine yeyote
ili kutoa taarifa,” alisema.
Alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo bado vimeendelea
kushika kasi ni pamoja na mauaji ya wivu wa kimapenzi, ukeketaji,
mauaji ya vikongwe, rushwa ya ngono makazini, wajane, unyanyasaji
majumbani na makazini.
Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali linalopinga masuala ya
ukeketaji kwa mwanamke (NAFGEM), Francis Selasini, alisema bado
wanawake wanaongoza kwa kufanyiwa vitendo vya ukatili, lakini pia
mitandao kwa sasa imeanza kupokea taarifa za wanaume wanaofanyiwa
vitendo hivyo.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo Kanda ya
Kaskazini, Elizabeth Mushi, alisema watazitumia siku hizo kutoa elimu,
kuhamasisha watu na kutoa msaada wa kisheria.
CHANZO:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment