Home »
» MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA TATU WA AFRIKA NA ARABIA, NCHINI KUWAIT, 20 NOVEMBA, 2013
Mfalme,
Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah, Amiri wa nchi ya Kuwait na
Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa tatu wa Afrika na Arabia;
Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn,
Waziri Mkuu wa Ethiopia na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa tatu wa Afrika na Arabia;
Waheshimiwa Wafalme na Koo za Kifalme;
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali;
Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa nchi za Kiarabu;
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Mwanzo
kabisa, nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe Mheshimiwa
Mfalme Sheikh Sabah Al-Ahmad Sabah, Amiri wa nchi ya Kuwait, Serikali na
wananchi wa Kuwait, kwa mapokezi mazuri na maandalizi makubwa
mliyofanya ya kuandaa mkutano huu. Pili, niruhusu nitoe salamu kutoka
kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ambaye alipenda sana kuhudhuria mkutano huu, lakini hakuweza
kufanya hivyo kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine ya kimataifa.
Mheshimiwa Rais amenituma kuwasalimu na pia kuwaeleza kuwa anautakia
mkutano huu mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Waheshimiwa Viongozi;
Nchi
za Afrika na Arabia zinaunganishwa na mambo kadha wa kadha yakiwemo;
historia, jiografia na utamaduni. Mahusiano yetu ya kihistoria na
ukaribu wa kijiografia yametusaidia kuwasiliana kwa karne nyingi.
Mawasiliano haya na mahusiano hayo, yamekuwa katika Nyanja za biashara,
dini na tamaduni. Leo hii, theluthi mbili ya idadi ya wakazi wenye asili
ya Arabia wanaishi Afrika. Nchini Tanzania, idadi kubwa ya wananchi
wetu walio ughaibuni wanapatikana katika nchi za ukanda wa Arabia.
Hakuna maeneo mengine nje ya Afrika ambapo lugha ya Kiswahili
inazungumzwa kwa ufasaha kama ilivyo kwa nchi za Oman na Yemen. Hizi ni
baadhi ya sababu zinazochangia kufanya ushirikiano baina yetu kuwa wa
lazima.
Kama
ambavyo tunaelewa, mkutano wa pili wa Afrika na Arabia uliofanyika
Libya mwaka 2010 uliazimia mambo mengi ya msingi yaliyolenga kukuza na
kutanua uhusiano baina ya kanda zetu hizi mbili. Kwa leo nitazungumzia
kupitishwa kwa mkakati Kazi wa Afrika na Arabia yaani (Africa-Arab
Strategic Framework and its Joint Plan of Action wa mwaka 2011 – 2016.
Mkakati huu ulibainisha maeneo manne ya mashirikiano ambayo ni:
ushirikiano wa kisiasa na uchumi, biashara na mtaji, kilimo na chakula
na mahusiano ya kijamii na kitamaduni.
Ndugu Waheshimiwa;
Ni
miaka mitatu sasa tangu tuanze kutekeleza mpango wa utekelezaji wa
Pamoja kwa nchi za kanda hizi na ripoti zilizowasilishwa katika mkutano
huu leo, zinaonesha bila kuficha yale tuliyofanikiwa kuyatekeleza.
Miradi mingi ya Maendeleo iliyopitishwa haijaanza kutekelezwa na baadhi
ndiyo iko katika hatua za awali ambapo hali hii imetokana na sababu
mbalimbali.
Ripoti ya pamoja ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa
Afrika (AU) na ile ya Sekretarieti ya Umoja wa nchi za Kiarabu imeeleza
kwa kina sababu zilizochangia kutotekelezwa kwa miradi mbalimbali
iliyopangwa.
Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na; ukosefu wa fedha za
uendeshaji, kutokuwepo mkakati wa ukaguzi na kushirikisha kwa kiwango
cha chini sekta binafsi. Ukitazama changamoto hizi, nyingi ziko chini ya
uwezo wetu na kupitia ushirikiano huu tunaweza kabisa kuzikabili katika
kipindi tunachoweza kujiwekea.
Ndugu Waheshimiwa;
Wote
tunafahamu kuwa dunia inapitia changamoto mbalimbali zikiwemo: athari
za mdororo wa uchumi, upungufu wa chakula, majanga yanayotokana na hali
ya hewa, kutokutangamaa kwa baadhi ya nchi sambamba na suala la ugaidi.
Changamoto hizi ni kubwa na ngumu ambazo haziwezi kukabiliwa na taifa
moja peke yake.
Kutokana na hali hii, kunahitajika mashirikiano baina ya
nchi za Afrika na Arabuni katika kipindi hiki kuliko ilivyokuwa huko
nyuma.
Kwa kuwa na mashirikiano haya, kanda zetu hizi zitakuwa
hazizungumzii tu changamoto zilizopo, bali pia zitaweza kukabiliana na
changamoto hizo kwa kutumia fursa zilizopo na hivyo kufanikisha matakwa
ya wananchi wa kanda hizi.
Nakushukuruni sana kwa Kunisikiliza!
0 comments:
Post a Comment