WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda, amezishauri nchi zote za Afrika kuridhia mikataba
ya uanzishwaji wa Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika iliyopo mjini
Arusha ili kutoa fursa kwa makundi, taasisi binafsi na raia kuitumia
mahakama hiyo pindi ukiukwaji wa haki za binadamu unapofanywa katika
nchi zao.
Pinda alitoa wito huo mjini hapa jana alipofungua semina ya siku tatu
ya wakuu wa vyombo vya sheria na majaji kutoka nchi wanachama wa Afrika
na taasisi za kimataifa za kisheria iliyoandaliwa na Mahakama ya Afrika
ya Haki za Binadamu.
Mpaka sasa ni nchi 26 barani Afrika zilizoridhia uanzishwaji wa
mahakama hiyo huku nchi saba zikitoa fursa kwa taasisi binafsi na hata
mtu mmoja mmoja kuwa na uwezo wa kufungua shauri katika mahakama hiyo
ikiwemo Tanzania.
Alisema ni vema nchi zote zikaridhia ili kutoa wigo mpana wa si tu wa
demokrasia katika nchi zao, bali kutoa fursa kwa raia wa kawaida kuwa
na haki ya kushtaki katika mahakama hiyo kama nchi yake na mahakama ya
nchi yake imekiuka moja ya haki za binadamu.
“Sisi kama Tanzania tumeridhia mkataba huo na kwa kiasi kikubwa
tunautekeleza kwa vitendo ndiyo maana hata waziri mkuu alipotoa matamko
ambayo baadhi ya asasi binafsi za kisheria zikadhani amekiuka moja ya
haki za binadamu wakaamua kufungua jalada mahakamani na kesi
inaendelea,” alisema Pinda.
Akieleza malengo ya semina hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Othmani
Chande, alisema majaji na wakuu wa mahakama mbalimbali Afrika na baadhi
ya nchi nyingine walioshiriki wanataka kushauriana jinsi ya kuweza kuwa
na tafsiri iliyo sawa juu ya haki za binadamu.
Alisema hivi sasa kila nchi inalinda haki za binadamu kupitia katiba
zao, lakini wakaona ni bora wakashirikishana kuwa na tafsiri moja juu ya
haki za binadamu katika mataifa yote ya Afrika.
Akizungumzia suala la viongozi wa Afrika kupelekwa katika Mahakama ya
Kimataifa ya Uhalifu (ICC), alisema tayari nchi za Afrika zimeomba
mkataba wa Roma upitiwe upya kutoa nafasi kwa mahakama za kanda za
Afrika kushughulikia kesi hizo.
Rais wa mahakama hiyo, Jaji Sophia Akuffo, alisema nchi za Afrika
haziwezi kuwa na amani ya kudumu kama suala la haki za binadamu
halitazingatiwa.
0 comments:
Post a Comment