Kiwango cha ufaulu chaongezeka asilimia 19.9
Kiwango cha ufaulu matokeo ya Darasa la Saba mwaka huu kimeongezeka kwa asilimia 19.89 huku wavulana wakiwabwaga wasichana.
Dk. Msonde alisema jumla ya watahiniwa 13 wamefutiwa matokeo yao baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 30.17 mwaka jana hadi asilimia 50.61, mwaka huu .
Akitangaza matokeo hayo juzi jijini Dar es
Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk.
Charles Msonde, alisema jumla ya watahiniwa 427,606 kati ya 844,938
waliofanya mtihani huo walipata alama zaidi ya 100 katika alama 250.
Alisema idadi hiyo ni sawa na asilimia
50.61 ambapo kati yao wavulana ni 219,379 sawa na asilimia 55.01 na
wasichana ni 208,227 sawa na asilimia 46.68.
Alisema miongoni mwao wamo wenye ulemavu
476 ambapo wasichana ni 219 sawa na asilimia 46.01 na wavulana ni 257
sawa na asilimia 53.99.
UFAULU KIMASOMO
Alisema watahiniwa walifanya masomo matano ambayo ni Kiswahili, Kiingereza, Maarifa ya Jamii, Hisabati na Sayansi.
Dk. Msonde alisema takwimu zinaonyesha
ufaulu katika masomo yote umepanda kwa asilimia kati ya 6.01 na 28.06
ikilinganishwa na mwaka jana.
Alisema matokeo yanaonyesha somo la
Kiswahili limeongoza kwa kuwa na ufaulu wa juu kwa asilimia 69.06 na
somo walilofaulu kwa kiwango cha chini zaidi ni hisabati lenye ufaulu wa
asilimia 28.62.
Alisema mwaka jana somo la Kiswahili ufaulu ulikuwa ni asilimia 41 na Hisabati ni asilimia 18.74.
Aliongeza kuwa katika somo la Kiingereza
ikilinganishwa na mwaka jana ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 21.06 na
kufikia 35.52 wakati somo la Maarifa ya Jamii ufaulu ulikuwa asilimia
28.61 na umefikia asilimia 53.00.
Alisema somo la Sayansi kwa mwaka jana ufaulu ulikuwa ni kwa asilimia 41.48 na mwaka huu umefikia asilimia 47.49.
WAFUTIWA WATOKEO
Dk. Msonde alisema jumla ya watahiniwa 13 wamefutiwa matokeo yao baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo.
Alisema kati ya idadi hiyo watahiniwa
watano walibainika walishawahi kufanya mtihani wa mwaka 2011/12 na
wanane walikutwa na vikaratasi vya majibu.
Aliongeza kuwa, idadi hiyo ya watahiniwa
waliofutiwa matokeo kwa mwaka huu ni ndogo ikilinganishwa na ya mwaka
jana ambapo jumla yao ilikuwa ni 293.
Kutokana na hilo, Baraza limeipongeza
Kamati za Uendeshaji Mitihani za mikoa, wilaya na walimu na wanafunzi
waliofanya mitihani hiyo.
Alisema baraza limewasilisha matokeo hayo
kwa mamlaka zinazohusika ili zifanye uchaguzi wa watahiniwa wa kujiunga
na elimu ya sekondari.
Alisema matokeo ya uchaguzi wa watahiniwa yatatangazwa na mamlaka husika mara baada ya kazi ya uchaguzi itakapokamilika.
Alisema matokeo ya mtihani huo yatawekwa kwenye tovuti za baraza, wizarani na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema ili kujiridhisha na usahihi wa
zoezi la usahihishaji kwa kutumia mfumo wa kompyuta, sampuli ya karatasi
20,795 ya majibu ya watahiniwa wa shule 200 kutoka katika wilaya 48 za
mikoa tisa zilisahihishwa kwa mkono.
Alitaja mikoa hiyo kuwa ni Iringa, Kagera, Shinyanga, Manyara, Njombe, Mbeya, Morogoro, Katavi na Tanga.
Alisema ulinganifu baina ya alama za
watahiniwa zilizopatikana kwa kusahihishwa kwa mkono na zile
zilizotokana na usahihishaji wa kompyuta ulifanyika na kubaini kuwa ule
wa kompyuta ulikuwa sahihi.
"Usahihishaji wa kutumia kalamu ulibainika
kuwa na makosa machache ya kibinadamu, kama kukosea kusahihisha swali
kwa kufuata mwongozo wa usahihishaji na dosari ya ujumla wa alama,"
alisema.
Alisema kati ya sampuli ya karatasi za watahiniwa 20,795, jumla ya karatasi 249 sawa na asilimia 1.2 zilibainika kuwa na makosa.
SHULE BINAFSI
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa
Shule Binafsi, Tamongsco Taifa , Mahmoud Mringo, akitaja mchanganuo wa
ufahulu wa masomo wa shule binafsi alisema Kiswahili ni asilimia 98,
Kiingereza ni asilimia 99, Maarifa ya Jamii ni asilimia 86, Hisabati ni
asilimia 81 na Sayansi ni asilimia 84 .
SOURCE:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment