Home » » VIGOGO WA SERIKALI WAONGOZA MIGOGORO YA ARDHI ZANZIBAR

VIGOGO WA SERIKALI WAONGOZA MIGOGORO YA ARDHI ZANZIBAR

Written By kitulofm on Tuesday, 31 December 2013 | Tuesday, December 31, 2013


Na Shariff Mbukuzi, Zanzibar

VIONGOZI wa nafasi za kisiasa Zanzibar wamethibitika kujiingiza katika fedheha kubwa kutokana na ulafi wa kumiliki ardhi.

Uchunguzi wa migogoro mbalimbali ya ardhi uliofanywa na kamati teule ya Baraza la Wawakilishi umebaini kuwa viongozi waandamizi serikalini na katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepewa maeneo kimabavu. Kwa mujibu wa ripoti ya kamati hiyo iliyoongozwa na Mwakilishi wa Kuteuliwa, Ali Mzee Ali, ugawaji wa ardhi kwa viongozi kadhaa ulifanywa kinyume cha sheria za ardhi za Zanzibar.
“Waliotajwa ambao tulipowaita wafike mbele ya kamati yetu walishindwa kutoa vielelezo vya namna walivyomilikishwa maeneo ya ardhi, ni pamoja na viongozi na baadhi ya watoto wa viongozi,” Baraza liliambiwa na Mzee alipokuwa akiwasilisha ripoti hiyo, wiki iliyopita.

Baraza liliazimia kuundwa kamati ya uchunguzi ili kuchunguza malalamiko ya wananchi yaliyolifikia baraza hilo kupitia kwa wajumbe wake, baada ya kuwepo tuhuma za kufutwa kwa hatimiliki za baadhi ya maeneo pasina kufuatwa sheria zilizopo.
Baadhi ya maeneo yaliyolalamikiwa – yakiwemo kwenye maeneo ya karibu na fukwe za Bahari ya Hindi – yalikuwa yakitumiwa na wananchi kwa kuchimba mchanga wa kujengea, na mengine kwa shughuli za kilimo.

Hadidu rejea zilizopangwa kufanyiwa kazi katika uchunguzi wa kamati teule ya Baraza, ni kuangalia mgogoro wa ardhi baina ya serikali, wananchi na wakulima wa kijiji cha Bambi, Wilaya ya Kati; mgogoro wa mfanyabiashara na wakulima wa kijiji cha Tumbe, Wilaya ya Micheweni; mgogoro wa wananchi na serikali iliyoyatoa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa vitega uchumi kijiji cha Makangale, Wilaya ya Micheweni na mgogoro baina ya wananchi na viongozi wa serikali eneo la Mchangamle, Kizimbani, Wilaya ya Wete.
Migogoro mingine ya ardhi iliyochunguzwa ni uliohusu wananchi wa Vitongoji Makaani, Wilaya ya Chake Chake; ule uliohusu mwekezaji na wananchi kijiji cha Pwanimchangani, Wilaya ya Kaskazini B; mwingine uliohusu wananchi na viongozi wa ngazi ya juu serikalini eneo la Tondooni Mkunguni, Pemba.
Mgogoro baina ya Idara ya Upimaji na Ramani na Wizara ya Kilimo eneo la Tumbe, Wilaya ya Micheweni ambao umetoa mwanya kwa wananchi kuvamia eneo hilo kwa shughuli za kilimo; mgogoro baina ya mwekezaji na wananchi eneo la Mzwardini, kijiji cha Bwejuu, Wilaya ya Kusini, Unguja.
Uchunguzi umebaini kwamba sheria za ardhi zimekiukwa na watendaji wa serikali kutajwa kama waliotoa mchango mkubwa katika uvunjaji wa sheria za ardhi.
Kamati ya uchunguzi ya Baraza la Wawakilishi ilibaini kuwa baadhi ya hatimiliki zilifutwa bila ya taratibu za kisheria, ikiwemo kumuarifu mmiliki wa awali kuhusu nia ya serikali kutwaa eneo.
Kwa mfano, uchunguzi umebaini, katika eneo linalogombaniwa na mwananchi aitwaye Ali Muradi na kampuni ya Zanzibar Dairy Products, mwekezaji alimilikishwa eneo hilo bila ya hati ya mwananchi kufutwa.
Katika mgogoro huo, kamati imesema, mawaziri wawili walioshika wadhifa wa wizara ya ardhi, walitoa hati ya kufuta kwa muda umiliki wa eneo kwa mmiliki wa awali, mwananchi, na kutoa hati mpya kwa mwekezaji huyo.
Kamati imesema si jambo la kawaida serikali kuidhinisha mmiliki aliyefutiwa hatimiliki ya eneo moja, kupatiwa eneo jingine kama ilivyotokea kwa mgogoro huo. Muradi alipewa eneo jingine na wizara ingawa sababu ya kufutiwa milki eneo la awali, ilielezwa kuwa ni kushindwa kuliendeleza.
“Utaratibu huo si wa kawaida kwa anayefutiwa hati kupatiwa eneo jengine, huku wizara hiyo katika taarifa yake kwa Kamati ilieleza kuwa eneo hilo lilifutwa kutokana na kuwahi kupewa mtu mwengine na hivyo kuamua kufuta hati ya Muradi kwa msingi huo. “Kamati baada ya kuitaka Wizara kuwasilisha kwao hati ya matumizi ya ardhi iliyotolewa awali, ilishindwa licha ya kuandikiwa barua mara kadhaa hadi wakati kamati ikikamilisha kazi yake,” alisema mwakilishi Mzee.
Akizungumzia mgogoro wa mfanyabiashara na wakulima wa kijiji cha Tumbe, Wilaya ya Micheweni, mwenyekiti wa kamati hiyo ya uchunguzi ya Baraza la Wawakilishi alisema mwaka 2010 kamati ya kudumu ya baraza (Kamati ya Mawasiliano) ilitembelea eneo hilo na kuagiza asilimia 70 ya eneo hilo wapatiwe wananchi ambao wamekuwa wakitumia eneo hilo kwa kilimo.
Hata hivyo, alisema serikali kupitia wizara ya ardhi, haikuzingatia agizo hilo. Matokeo yake, kamati ilikuta, eneo kubwa waligawiwa viongozi wa juu serikalini, na kuwataja mawaziri, spika wa baraza, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na wakuu wa kamati za ulinzi na usalama wa maeneo hayo.
Ripoti ya kamati imetaja kwa majina viongozi waliopewa ardhi eneo la Tumbe kuwa ni Shamsi Vuai Nahodha (Mwakilishi wa Mwanakwerekwe na Mbunge wa Kuteuliwa), Mbunge wa Uzini, Muhammed Seif Khatib na Mbunge wa Makunduchi, Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano.
Majina mengine yaliyotajwa katika ripoti hiyo ni wanasiasa wakongwe wa jimbo la Donge, Ali Ameir Mohamed na Ali Juma Shamhuna (waziri katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Zanzibar), Suleiman Othman Nyanga (Mwakilishi wa Jang’ombe na waziri), Asha Abdalla Juma, aliyekuwa waziri serikali, Amani Karume sasa akiwa mjumbe wa Sekretarieti ya CCM na Dk. Maua Daftari, mbunge Viti Maalum (CCM) mwenyeji wa Wete, Pemba.
Katika mgogoro wa ardhi baina ya wawekezaji eneo la Matemwe, Wilaya ya Kaskazini A, kamati ilibaini kuwa mwekezaji kampuni ya Al Nakheel, aliyekodishwa eneo awali kujenga hoteli, alifutiwa hatimiliki kwa madai ya kushindwa kuliendeleza.
Kamati iliona katika uchunguzi wake kuwa kulikuwa na barua ilizoandikiwa kampuni ya Leisure Corp kujulishwa kufutiwa hatimiliki siku moja na kuhalalishwa kwa eneo hilo kwa kampuni nyingine tatu kutumia eneo husika.
Maofisa wa wizara waliiambia kamati kwamba hatimiliki za kampuni tatu baadaye, zilifutwa kwa sababu miradi yao haikuidhinishwa kisheria kutokana na kutopitishwa na Mamlaka ya Uwekezaji Vitegauchumi Zanzibar (ZIPA). ZIPA imeanzishwa kwa Sheria ya mwaka 1992, na uidhinishaji wa miradi ya vitegauchumi hufanywa kupitia Kifungu 46(3) kinachohusu matumizi ya ardhi kwa shughuli za uwekezaji vitegauchumi.
Kamati katika hatua nyingine ikielezea uamuzi wa serikali kufuta hati ya ukodishaji wa ardhi eneo la Uroa kwa mwekezaji Bruno Konti kwa muda wa miaka 33, ilisema imebaini kuwa badala yake eneo hilo walilojenga hoteli, alimilikishwa mtoto wa waziri katika serikali aliyoongoza Amani Abeid Karume.
Hata hivyo, hakuna kielelezo hata kimoja wala maelezo ya mdomo yaliyotolewa na maofisa wa wizara kuthibitisha uamuzi huo kwa maandishi kama sheria inavyotaka.
Mwakilishi Mzee alisema katika kuwasilisha ripoti ya uchunguzi kuwa kamati yake ilibaini ukiukaji mkubwa wa taratibu za kukodisha visiwa vidogo vya kitalii nje ya bandari ya Malindi, Zanzibar.
Baadhi ya waliokodishwa walitozwa kiwango kidogo cha fedha za kukodi, kuliko waombaji wengine waliokuwa tayari kulipa fedha nyingizaidi. Miongoni mwa mapendekezo ya Kamati ya Mzee ni serikali kurudisha umilikaji wa maeneo kwenye himaya yake na kutangaza ukodishaji ili wanaotaka kuwekeza waombe rasmi.
Chanzo: Fahamu
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

KITULO FM LOGO

KITULO FM LOGO
Tusikilize masaa 18 kwa siku kupitia masafa ya 97.0 FM ukiwa wilayani Makete mkoani Njombe na maeneo ya jirani

WASOMAJI WETU

KUMBUKUMBU YA HABARI ZETU

 

Copyright © 2013. KITULOFM BLOG - Haki zote zimehifadhiwa
Imetengenezwa na Edwin Moshi
Inawezeshwa na Kitulo Fm