IRINGA
Ujenzi wa kituo cha Mabasi cha Igumbilo Manispaa ya Iringa umesitishwa baada
ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Dk.
Binilith Mahenge kuamuru tathimini ya athari ya mazingira ifanywe upya.
Waziri amefikia uamuzi huo baada ya kutembelea eneo la ujenzi wa kituo hicho
kufuatia kupata malalamiko juu ya athari za kujenga kituo hicho kutoka kwa
Wizara ya maji, Mkoa wa Iringa na Mamlaka ya maji safi na maji taka mjini Iringa
(IRUWASA) kuwa ujenzi wa kituo hicho utaathiri afya za watumiaji wa maji wa
Iringa.
Dr mahenge amesema ni vyema
Halmashauri ya Manispaa hiyo kusitisha shughuli zote za kuendeleza eneo hilo
kusubiri maamuzi ya serikali.
Aidha ameongeza kuwa hawezi kulitolea uamuzi suala la ujenzi wa kituo hicho
bila kuwashirikisha wataalamu na kumuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la
Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Bonaventura Baya kurudia kufanya tathimini upya
ili kubaini tatizo lilopo pamoja na madhara yatakayojitokeza.
Naye Mkurugenzi wa NEMC , Baya anasema watafanya tathimini hiyo kwa muda wa
wiki mbili na kuhakikisha kuwa majibu yatakuwa tayari ili kuweza kusaidia
maamuzi kutolewa mapema kwa kufuata ushauri wa wadau mbalimbali juu ya ujenzi
huo wa stendi ya Igumbilo.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi amesema
ni vyema haki ikatendeka ili jambo hilo lisichukuliwe na kuonekana ni suala
lenye maslahi ya kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amesema kuwa kinachotakiwa
ni kufanya subira ya matokeo ya NEMC na maamuzi ya serikali na kuwa kujenga au
kutojenga kituo hicho ni maamuzi yatakayotolewa na serikali.
Akitoa Taarifa kwa waziri, Katibu Tawala wa Mkoa, Wamoja Ayubu anasema kuwa
ujenzi wa kituo hicho ni mzuri na unadhana ya kuboresha miundombinu ya Manispaa
ya Iringa, kukuza uchumi pamoja na kuvutia wawekezaji.
Aidha Wamoja anasema maji ya mto ruaha ni chanzo muhimu cha maji kwa wakazi
wa Manispaa ya Iringa na kuwa IRUWASA imewekeza zaidi ya Sh70 Bilioni kwenye
mto huo ili kuwapatia wananchi maji safi.
Iruwasa wanadai kuwa ujenzi wa kituo hicho utaendanana na shughuli za
kibiashara na gereji jambo litakaloathiri maji kwa kuwa chujio zilizofungwa
hazina uwezo wa kuchuja tqaka kemikali.
Wamoja
alisema kuwa ujenzi huo endapo utatiririsha maji machafu taka ngumu na kemikali
itaathiri maji ya mto Ruaha na pia itasababisha wakazi wa Iringa kuwa hatarini
kutokana na kunywa maji yasiyo salama.
0 comments:
Post a Comment