Wazazi hao wa wilaya ya Muleba walishindwa kuwapeleka shuleni watoto wao waliochaguliwa kujiunga na sekondari walipokamatwa na polisi kwa agizo la Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa wilaya hiyo Lembris Kipuyo, alisema wazazi hao wamekamatwa baada ya kukaidi agizo lake la kuwataka kuwapeleka wanafunzi shuleni mara moja, hata kama hawana ada na vifaa vinavyohitajika.
Alisema msako wa kuwakamata wazazi wengine ambao mpaka sasa hawajawapeleka watoto hao shule unaendelea katika kata zote za wilaya hiyo ili waweze kufikishwa katika vyombo vya dola.
Kipuyo alisema kati wa wanafunzi 7,894 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wilayani humo kabla ya agizo lake la wiki iliyopita, ni wanafunzi 898 pekee waliokuwa wameripoti kujiunga katika shule 52 za serikali.
Hata hivyo alisema kuwa baada ya kuanza kwa msako huo, idadi ya wanafunzi hao imeongezeka ndani ya wiki moja hadi kufikia 5,641.
Kipuyo aliwasisitiza wazazi na walezi ambao watoto hawajajiunga na kidato cha kwanza, kuwapeleka mara moja hata kama hawana ada na vifaa vya shule ili waweze kupatiwa utaratibu wa kutafuta michango hiyo wakati wakiendelea na masomo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment