WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikitamba kupata ushindi wa kura
20,828, sawa na 86.61% katika uchaguzi mdogo Chalinze, Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeibuka na madai kwamba mgombea wa
CCM, Ridhiwani Kikwete, alitoa rushwa.
CHADEMA imetoa kauli hiyo ikiwa ni sehemu ya tamko la awali kwa umma
kuhusu kile ilichodai kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu, kanuni na
sheria zinazosimamia uchaguzi, zilizofanyika kwenye mchakato wa uchaguzi
mdogo Chalinze, ambao umehitimishwa jana na mtoto wa Rais Jakaya
Kikwete, Ridhiwani kuibuka mshindi.
Katika taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana, CHADEMA
kupitia Mkuu wa Operesheni ya Uchaguzi Mdogo-Chalinze, John Mrema,
ilisema kuwa Ridhiwani aliwatumia makuwadi wake kumshawishi
mgombea wa CHADEMA ajitoe kwa ahadi ya kupatiwa cheo atakachokuwa
tayari, kati ya ukuu wa mkoa au wilaya, mahali popote nchini.
“Vishawishi vya rushwa kwa ajili ya kujitoa, kinyume na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kifungu cha 91B, ambacho kinasema:
“Mtu yeyote atakayemshawishi au kumsababisha mtu mwingine kujitoa kuwa mgombea katika uchaguzi kwa kupewa malipo, ukuwadi wa malipo au ahadi ya malipo na mtu yeyote…atakuwa amefanya kosa la rushwa na iwapo atatiwa hatiani atatumikia kifungo kisichozidi miaka mitano,”
“Mgombea wa CCM aliwatumia makuwadi wake kumshawishi mgombea wa
CHADEMA ajitoe kwa ahadi ya kupatiwa cheo atakachokuwa tayari, kati ya
ukuu wa mkoa au wilaya, mahali popote nchini,” ilisema taarifa hiyo ya
CHADEMA.
CCM kufanya kampeni siku ya uchaguzi
CHADEMA kwenye taarifa hiyo ililalamikia ukiukwaji wa sheria na
kanuni za uchaguzi zilizofanywa na Rais Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CCM.
CHADEMA imedai kuwa Rais Kikwete alivunja sheria kwa kufanya kampeni
siku ya kupiga kura, akiwa kwenye kituo cha kupigia kura, ambapo
alinukuliwa na na kutangazwa moja kwa moja kupitia vyombo mbalimbali vya
habari, akisema yeye amempigia kura mgombea wa CCM.
“Kitendo hicho cha Rais Kikwete ambacho kililenga kufanya kampeni,
kushawishi na kuelekeza wapiga kura, ni kinyume cha Sheria ya Uchaguzi,
kifungu cha 104 (1), ambacho kinasema:
“Hakuna mtu atakayefanya mkutano siku ya kupiga kura au; ndani ya jengo lolote ambamo upigaji kura katika uchaguzi unaendelea, au mahali popote ndani ya eneo la mita 200 ya jengo hilo…kuonesha upendeleo au nembo nyingine inayoonesha kuunga mkono mgombea fulani katika uchaguzi.”
Kifungu cha 104 (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kinasema:
“Mtu yeyote atakayekwenda kinyume na kifungu hiki, atakuwa amefanya kosa…”
0 comments:
Post a Comment