Mratibu
wa Mtandao wa Utepe Mweupe Kitaifa (The White Ribbon Alliance), Rose
Mlay akimjulia hali mmoja wa akinamama aliyejifungua katika wodi ya
wazazi katika Kituo cha Afya Kibiti leo.

Mratibu
wa Mtandao wa Utepe Mweupe Kitaifa (The White Ribbon Alliance), Rose
Mlay akitambulishwa kwa baadhi ya wahudumu katika wodi ya wazazi kwenye
Kituo cha Afya Kibiti leo alipotembelea kuangalia mwenendo wa utoaji
huduma za dharura katika kituo hicho.

Jengo ambalo ni chumba cha upasuaji linalotoa huduma za dharura kwa wajawazito katika Kituo cha Afya Kibiti.

Mmoja
wa akinamama aliyepatiwa huduma za uzazi katika Kituo cha Afya Kibiti
kinachotoa huduma za dharura kwa akinamama wajawazito akizungumzia
msaada wa huduma hiyo kwa wajawazito.

Mganga
Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kibiti, Chagi Jonas Lymo akizungumza na
mwandishi wa habari wa Kituo cha ITV alipotembelea kituo hicho pamoja na
Mtandao wa Utepe Mweupe Kitaifa (The White Ribbon Alliance).
Baadhi ya akinamama wakipatiwa huduma katika kituo cha afya Kibiti jana.

Mratibu
wa Mtandao wa Utepe Mweupe Kitaifa (The White Ribbon Alliance), Rose
Mlay (kulia) akizungumza na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kibiti,
Chagi Jonas Lymo katika kituo hicho leo Kibiti.
MGANGA
Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kibiti, Chagi Jonas Lymo amesema uwepo wa
huduma za dharura kwa wajawazito katika kituo hicho cha afya umesaidia
kiasi kikubwa katika uokoaji wa maisha ya mamamjamzito pamoja na vifo
vya watoto eneo hilo.
Lymo ametoa
kauli hiyo leo mjini Kibiti alipokuwa akizungumza na Mratibu wa Mtandao
wa Utepe Mweupe Kitaifa (The White Ribbon Alliance), Rose Mlay pamoja
na Mkurugenzi wa World Lung Foundation walipotembelea kituo hicho
kuangalia namna kinavyotoa huduma kwa wananchi na changamoto zake.
Akizungumza
zaidi, Lymo alisema tangu Kituo cha Afya cha Kibiti kuanza kutoa huduma
za dharura kimekuwa msaada mkubwa kwa akinamama wajawazito eneo hilo na
kwa sasa idadi ya akinamama wanaojifungulia eneo hilo imeongezeka mara
tatu zaidi tofauti na ilivyo kuwa awali jambo ambalo unaonesha
wamevutiwa na huduma hiyo muhimu kwa wajawazito.
Alisema kwa
sasa kituo hicho kinafanya upasuaji kwa matatizo yote ya uzazi kwa
wajawazito, ikiwemo kutoa huduma za kuongezewa damu kwa wajawazito wenye
mahitaji jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya
mama mjamzito pamoja na mtoto mtarajiwa.
“…Awali
tulikuwa hatutoi huduma za upasuaji kwa akinamama wajawazito…tulikuwa
hatuna chumba cha upasuaji hivyo tulitoa huduma za uzazi za kawaida, na
ilipotokea matatizo kwa mjamzito tulimshauri kwenda ama kwenye hospitali
ya Mchukwi (ya kulipia) ambayo ipo umbali wa takribani kilometa 15 au
kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya Utete ambayo ni kilometa 84 kutoka
hapa,” alisema.
“…Baada ya
kuanzisha huduma za upasuaji kwa akinamama wajawazito, akinamama
waliokuja kujifungulia hapa waliongezeka…, mwezi wa kwanza tu wa kuanza
kutoa huduma hizi wakinamama waliongezeka kutoka idadi ya wagonjwa 35
kwa mwezi waliongezeka hadi kufikia zaidi ya akinamama 100 kwa mwezi,”
alisema Lymo.
Alisema kwa
mwezi uliopita (Machi) jumla ya wajawazito 135 walifika kupata huduma
za uzazi kiasi ambacho kwa sasa ni kikubwa na kinazidi uwezo wa kituo,
jambo ambalo alishauri ipo haja ya kituo hicho kuongezewa mahitaji anuai
ili kwenda sambamba na ongezeko la wateja wake kwa sasa.
Kwa upande
wake Mratibu wa Mtandao wa Utepe Mweupe nchini, Bi. Rose Mlay alisema
serikali ikiamua kwa kushirikiana na wadau wengine inaweza kumaliza
matatizo ya vifo kwa wajawazito pamoja na watoto kwa kusogeza huduma za
dharura katika vituo vya afya ambavyo vingi vipo karibu na wananchi.
“…Inawezekana
kabisa kupambana na vifo vya akinamama wajawazito pamoja na watoto
endapo Serikali ikijipanga na kuamua vituo vya afya viwekewe bajeti ya
kutosha na hatimaye kuweza kutoa huduma za dharura kwa akinamama
wajawazito na watoto,” alisema Bi. Mlay.
World Lung
Foundation ndiyo taasisi iliyokiwezesha kituo cha Afya cha Kibiti kuweza
kutoa huduma za dharura kwa akinamama wajawazito. Akizungumzia hatua
hiyo, Mkurugenzi wa World Lung Foundation, Dk. Nguke Mwakatundu alisema
taasisi hiyo imevisaidia jumla ya vituo 10 vya afya kutoa huduma za
dharura pamoja na kuziwezesha hospitali nyingine tano katika nyanja
tofauti kwenye utoaji huduma za afya.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com


0 comments:
Post a Comment