Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Yohana Sefue.
TAMKO LA KATIBU MKUU KIONGOZI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU HATI YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 14 APRILI, 2014
Siku
12 zijazo tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wamezaliwa
watu ndani ya Muungano huu na wengine wana wajukuu.
Inasikitisha sana kuwa leo, miaka 50 baadaye ipo dhana potofu
inayojengwa kuwa Muungano huu si halali kwa vile hakuna Hati ya Muungano
(Articles of the Union).
Waasisi wa Taifa letu ambao tarehe 22 Aprili, 1964 kule Zanzibar
walitia saini Hati hiyo, mbele ya mashuhuda, nao wameonekana kama
walichokifanya kilikuwa kiini macho, na kwa hiyo kwamba waliongoza Taifa
jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msingi wa kiini macho
hicho kwa miaka yote hadi Mwenyezi Mungu alipowaita.
Mambo yote mawili yametusononesha sana sisi Serikalini, na bila shaka
yamewasononesha wananchi wanaoipenda nchi yao, wanaowapenda Waasisi wa
Taifa letu na kuuenzi Muungano wao.
Madai ya kuonyeshwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi lakini
hatukuweza kuamini hali itafikiwa ilipofikia, ambapo wapo watu
wanathubutu kudai na kuapa kuwa Hati hiyo haipo.
Ukweli ni kuwa hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote. Hata hivyo, lazima
tukubaliane kuwa zipo Hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama
Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama
mboni ya jicho.
Hati hizo ni pamoja na Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya
mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962, na Hati ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964. Hati za aina hii
zinahifadhiwa maeneo maalum ambayo ni salama ili zisipotee wala
kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi, tunazifungua ili kuzihifadhi kwa
namna yoyote ile.
Lakini sasa maneno yanakua mengi, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka
zimekuwa nyingi, kiasi cha wananchi kuanza kutiwa mashaka iwapo kweli
Hati ya Muungano ipo au la.
Hivyo, kwa maagizo na ridhaa ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninaleta mbele yenu Hati ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi
wetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume, ili
muione na kuwahakikishia Watanzania kuwa yanayosemwa kuwa hakuna Hati
hiyo si kweli. Hati hiyo ipo tangu wakati huo, imetunzwa vizuri na
waliotutangulia, tumeirithi, na tutaendelea kuihifadhi.
Na, tukiombwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge Maalum nina uhakika
Rais ataridhia ipelekwe huko ili kuondoa mjadala wa kama Hati ipo au la.
Isitoshe, tufanye utaratibu wa kuweka nakala kwenye Makumbusho ya Taifa
ili kila atakayetaka kuiona katika miaka mingine 50 ijayo na kuzidi
aione.
Mwisho, narejea kusema kuwa kwa upande wa Serikali tunasikitishwa na
kufadhaishwa sana na tuhuma nzito kwamba labda waasisi wetu hawakuwa
makini au walitufanyia kiini macho. Hatukutarajia wawepo Watanzania
wenzetu, wafikie hapo.
Ni jambo zito. Vile vile hatukutarajia kuwa Serikali itatuhumiwa kuwa
haikuwa makini kuhifadhi waliosaini waasisi wetu.
Matumaini yetu ni kuwa baada ya leo tutaendelea na mambo ya msingi kwa
mustakabali, umoja na uimara wa Taifa letu badala ya kuchochea hisia
kuwa Muungano wetu hauna msingi imara wa kisheria.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
0 comments:
Post a Comment