Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Ndugu zangu,
Naziona ishara za kuendelea kwa mvumo mbaya wa upepo wa kisiasa na hususan inapohusu hoja ya Muungano na muundo wa Serikali.
Mjadala unaoendelea sasa ni kama vile umefunikwa kwa chandarua kisicho na kinga ya wadudu wenye madhara kama mbu.
Tunakoelekea
si kuzuri. Msimamo wangu uko wazi, kuwa tunahitaji muundo wa Serikali
Tatu ili tuimarishe Muungano wetu. Kwamba tunahitaji uwepo wa Tanganyika
kama nchi.
Lakini,
nahofia katika tofauti hizi za mitazamo, kuna wenye kuamini katika
Serikali Tatu lakini bila kuwa na nia njema kwa nchi.
Na kuna wenye
kuamini hivyo wakiwa na dhamira njema pia. Hivyo hivyo kwa wenye kuamini
katika Serikali Mbili.
Hivyo,
nimeipitia mara kadhaa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa
alipokuwa akifungua Bunge Maalum la Katiba.
Nimejitahidi kuitafuta
mantiki kwa alichokizungumza Rais wa Nchi. Naamini Jakaya Kikwete
aliongea kile alichokiamini moyoni mwake.
Kikwete alionyesha hofu juu ya
Serikali Tatu ingawa aliweka wazi kuwa maamuzi ya mwisho ni ya Wabunge
wenyewe. Ni haki ya Kikwete kama mwanadamu kuelezea hisia zake.
Lakini
, Jakaya Kikwete si kama Watanzania wengine. Ni Rais wa Nchi.
Nikifikiri leo, naamini ilikuwa sahihi kwa Kikwete kukisema
alichokisema, hata kama hakifanani na misimamo kama ya kwangu.
Maana,
nikiwasikiliza ndugu zetu wa Zanzibar , hasa wenye kuupinga Muungano
katika hali iliyopo, na jinsi wanavyojadili, kwa kweli natishikia pia.
Na hakika, kwa kuufuatilia mvumo wa upepo wa kisiasa unaoendelea sasa,
Jakaya Kikwete alitusaidia kuyaweka wazi mawazo yake binafsi. Maana,
ingawa Serikali Tatu na Tanganyika inahitajika, lakini, huu si wakati
wake.
Ni jambo la kusubiri lije tutakapokuwa tayari kama watu
tulioungana; Visiwani na Bara. Na tuanze sasa kufanya jitihada za
kuyatafuta maridhiano juu ya kwa nini haya ya kubadilli mfumo wa
Serikali kwenda Serikali Tatu wakati wake haujafika.
Maana,
kuendelea kujadili Serikali Tatu sasa ni kuzidi kuipeleka nchi yetu
tunayoipenda kwenye mgawanyiko na mpasuko mkubwa.
Ni busara nionavyo,
kuwa Wabunge wetu kule Dodoma watambue kuwa rasimu ya Jaji Warioba,
ukiacha muundo wa Muungano na mfumo wa Serikali , ina mengi sana ya
muhimu ili kututoa hapa tulipo na kuwasaidia wananchi.
Waitafute
busara ya kulisubirisha hili la Muuundo wa Muungano unaopendekezwa na
Rasimu ya Warioba na hata muundo wa Serikali. Tubaki na Serikali Mbili
na tuboreshe kinachoweza kuboreshwa.
Maana, si kila unachokigawa maana yake kuna kinachobaki. Kugawa pia kuna maana ya kumaliza pia.
Na mengine tuyafanyao katika wakati usio sahihi huzaa kutokuaminiana.
Na kwa mwanadamu pale mtaji wa imani unapomalizika, kinachobakia ni kumaliziana.
Usimwone nyani ana makovu ukadhani ni simba aliyemjeruhi. Nyani huishi kwa kumwogopa zaidi nyani mwenziwe.
Kugawanyika kwa shari ni kutawanya mitaji ya kuaminiana.
Na kitachobaki ni kuumizana, kwa kugombani kiduchu chunguni kilichogandiana…
Ni wakati sasa wa kutanguliza busara na hekima zitakazotunusuru na mpasuko mkubwa zaidi wa kijamii.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.
Maggid,
Iringa.
0 comments:
Post a Comment