Dodoma/Dar. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Tundu
Lissu amesema Tanganyika ilikufa kwa amri iliyotolewa na Mwalimu Julius
Nyerere na siyo kwa makubaliano katika hati ya Muungano.
Lissu alitoa kauli hiyo jana alipopata fursa ya
kukamilisha dakika 16 za hotuba yake ya ufafanuzi wa maoni ya walio
wachache iliyokuwa imekatishwa baada ya matangazo ya moja kwa moja ya
Televisheni ya Taifa (TBC1) kukatika Jumamosi iliyopita.
Huku akinukuu maneno yaliyopo katika vitabu
vilivyoandikwa na Profesa Issa Shivji na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa
CCM, Pius Msekwa, Lissu alisema Jamhuri ya Muungano ilizaliwa bila
uhalali wa kisheria kwa kuwa hayakuwapo makubaliano ya kila upande wa
Muungano.
Alisema Aprili 26, 1964 (Siku ya Muungano),
Mwalimu Nyerere alitoa amri ya masharti ya mpito ya mwaka 1964 ambayo
pamoja na mambo mengine iliifuta Tanganyika. Akichambua kitabu cha ‘50
Years of Independence: A Concise Political History of Tanzania’ (Miaka
50 ya Uhuru: Historia fupi ya Tanzania), kilichoandikwa na Msekwa na
kuchapishwa Januari mwaka huu, Lissu alisema:
“Msekwa anasema katika kitabu hicho kuwa amri hiyo
ilichapishwa katika Gazeti la Serikali la siku hiyo. Kwanza,
iliwabadilisha waliokuwa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika
kuwa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.”
Alisema hata Mahakama Kuu ya Tanganyika iligeuzwa
kuwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano na nembo ya Taifa ya Jamhuri ya
Tanganyika iligeuzwa kuwa nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema tarehe hiyohiyo, Mwalimu Nyerere alitoa
amri ya Katiba ya muda ya mwaka 1964 na ilitangaza kuwa Katiba ya
Tanganyika ndiyo iwe Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano.
“Kifungu cha nne cha amri hii ndicho kilichoipatia
Serikali ya Muungano majukumu kuhusu mambo yote ya Muungano katika
Jamhuri ya Muungano yote na vilevile kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano
kwa upande wa Tanganyika,” alisema Lissu huku akishangiliwa na baadhi ya
wajumbe wa Bunge hilo.
Alisema Juni 15, 1964, Mwalimu Nyerere alitoa amri
nyingine iliyoitwa ‘Amri ya Masharti ya Mpito’ ambayo ilieleza kwamba
mahali popote ambako sheria zilizokuwapo zimetaja jina la ‘Tanganyika’
basi jina hilo lifutwe na badala yake jina la ‘Jamhuri ya Muungano’
liwekwe.
Huku akimnukuu Msekwa, Lissu alisema kigogo huyo
wa CCM katika kitabu chake amesema, “Uhai wa Tanganyika ulitolewa kwa
njia hiyo ya amri.
Athari za jumla za amri hizi ni kwamba eneo la kisiasa ambalo ndiyo ilikuwa Tanganyika lilitolewa uhai wake moja kwa moja kwa amri. Hii ndiyo sababu hata jina la eneo la kijiografia lililojulikana zamani kama Tanganyika ilibidi libadilishwe na kuwa Tanzania Bara.”
Athari za jumla za amri hizi ni kwamba eneo la kisiasa ambalo ndiyo ilikuwa Tanganyika lilitolewa uhai wake moja kwa moja kwa amri. Hii ndiyo sababu hata jina la eneo la kijiografia lililojulikana zamani kama Tanganyika ilibidi libadilishwe na kuwa Tanzania Bara.”
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Lissu
aliyoitoa jana, Msekwa alisema: “Kitabu kipo na ukikisoma kwa umakini
utagundua kuwa alichokisema Lissu siyo ambacho kimeandikwa. Sasa umhoji
kuhusu hayo aliyoyasema, muulize ameyapata wapi?”
CHANZO:Mwananchi
CHANZO:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment