Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso.
MKUU wa Kituo cha Polisi Igunga, Tabora, SP Edson Mfuru, anayedaiwa
kumuachia kitatanishi mtuhumiwa Magaka Singu, amepandishwa cheo na
kuhamishiwa wilayani Pangani, Tanga kuwa Mkuu wa Upelelezi (OC CID).
SP Mfuru anadaiwa kumwachia Singu kati ya Novemba 10 na 11,
aliyefikishwa kituoni hapo kwa tuhuma za kumtia ujauzito mwanafunzi wa
darasa la sita mwenye miaka 16 katika Shule ya Msingi Hani Hani baada
ya kupewa sh milioni 3.4.
Wakati Mfuru akipandishwa cheo na kuhamishiwa kituo, Jeshi la Polisi
mkoani Tabora limekana kuitambua namba ya jalada la kesi yenye
utambulisho wa IG/RB1430/2013 iliyosababisha Singu kukamatwa kabla ya
kuachiwa katika mazingira ya utata.
Kwa sasa binti anayedaiwa kupewa ujauzito na Singu yupo kijijini kwao
Hani Hani wilayani Igunga akiwa ameacha shule bila kupata msaada
wowote kutoka kwa mtuhumiwa.
Mwishoni mwa mwaka jana, gazeti hili liliandika habari juu ya binti
huyo na kunukuu maelezo ya aliyekuwa mkuu wa polisi mkoa huo, Peter
Ouma ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es
Salaam.
Mkuu huyo alisema wanachunguza sakata hilo na watatoa majibu kwa viongozi wa ngazi ya juu wa jeshi hilo kwa hatua zaidi.
Habari hiyo ilimnukuu Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu,
aliyekemea utaratibu uliotumika kumuachia mtuhumiwa na kuahidi
kufuatilia kuhakikisha mkuu huyo wa kituo anaondolewa.
Hata hivyo, msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso,
alipoulizwa zaidi ya mara mbili juu ya hatma ya tuhuma zinazomkabili
mkuu huyo wa kituo, alisema suala hilo linapaswa kutolewa maelezo na
Kamada wa Polisi wa Mkoa.
Alisema majukumu ya polisi makao makuu ni ya kiutawala zaidi, huku
akiainisha kuwa suala la uhamisho kwa askari yeyote ndani ya jeshi ni
utaratibu wa kawaida wa kikazi.
Kamanda wa sasa wa polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, amekana
kuzitambua namba za RB hiyo kutumika kama kumbukumbu yao kwa Wilaya ya
Igunga.
Hata hivyo, taarifa nyingine kutoka ndani ya jeshi hilo wilayani
Igunga zinakiri kufahamu uwepo wa RB IG/1430/2013 na kueleza kuwa
imefanywa kuwa ya malalamiko ya mtu mwingine tofauti na waliyopewa
wazazi wa binti aliyetiwa ujauzito.
0 comments:
Post a Comment