VURUGU na kampeni chafu zinazofanywa na baadhi ya makada wa CCM
wanaojipanga kuwania ubunge katika jimbo la Tarime, zimechukua sura
mpya.
Hatua hiyo imetokana na mbunge wa jimbo hilo Nyambari Nyangwine
(pichani), kuweka bayana kuwa atawasilisha malalamiko kwa uongozi wa CCM
ngazi ya wilaya, mkoa na taifa.
Juzi, baadhi ya wanachama wa CCM wilayani Tarime, walilalamikia kampeni
chafu zinazofanywa na baadhi makada na kusababisha makundi ambayo ni
hatari kwa Chama.
Hata hivyo, baadhi ya makada hao ambao baadhi wametajwa kuungwa mkono na
baadhi ya viongozi wa CCM wilayani humo, wamekuwa wakieneza siasa chafu
za ukabila, jambo ambalo limeelezwa kuwa ni hatari.
Makada hao ambao baadhi walishindwa kwenye kura za maoni, ambapo sasa
wameanza kujipanga upya lakini wakitumia njia ambazo ni kinyume na
taratibu za CCM.
Taarifa ya Nyangwine kwa vyombo vya habari jana, imesema kuwa
atawasilisha malalamiko yake ikiwa ni pamoja na kuwataja kwa majina
makada hao. Imesema kuwa makada hao wamekuwa wakieneza siasa za chuki zenye lengo la kukwamisha utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Hata hivyo, alisema kamwe hatishwi na makada hao kwa kuwa baadhi
waligombea mara kadhaa na kushindwa hivyo jimbo hilo kutawaliwa na
wapinzani kwa miaka 10.
Alisema CCM ni chama chenye demokrasia na kinajali haki za kila
mwanachama katika kuwania uongozi, lakini kina taratibu zake ambazo ni
lazima zifuatwe ikiwa ni pamoja na kusbiri muda mwafaka wa kufanya
kampeni na si kuwahujumu waliopo madarakani.
“Nitawasilisha malalamiko yangu rasmi kwa uongozi wa chama ngazi zote
hadi kwa Katibu Mkuu wetu (Abdulrahaman Kinana), sasa hivi ni wakati wa
kutekeleza Ilani za Chama kwa wananchi si kufanya kampeni ili kukwamisha
kazi.
“Waniache nitumikie wananchi walionichagua na muda ukifika waje
tupambane kwa hoja ndani ya Chama, haya wanayoyafanya sasa hivi ni uhuni
na kutaka kurejesha makundi ambayo mwisho wa siku yatakigharimu chama
chetu.
“Baadhi ya wanaoendesha siasa hizi chafu ni wanasiasa ambao wameishiwa
sera na goigoi na ndio sababu wameshindwa mara kadhaa kwenye uchaguzi,”
alisema Nyangwine kwenye taarifa yake.
CHANZO:EDDY BLOG
0 comments:
Post a Comment