Mafuriko jijini Dar es Salaam, Tanzania
Idadi ya waliokufa kutokana na mafuriko jijini Dar es Salaam imefikia watu 13 kufikia Jumatatu.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadiq Meck Sadiq
amesema idadi hiyo huenda ikaongezeka baada ya kupata taarifa za matukio
ya mafuriko kutoka maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa siku tatu mfululizo tangu Ijumaa
iliyopita, mvua kubwa ziliendelea kunyesha na kusababisha madhara
makubwa vikiwemo vifo, uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja,
hivyo kukata mawasiliano na mikoa ya jirani ya Pwani na Morogoro na
hata ndani ya mkoa wenyewe.
Karibu maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam
yameathirika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha
mafuriko, huku wakaazi wa maeneo ya mabondeni wakiathirika zaidi baada
ya nyumba zao kujaa maji. Miundombinu ya barabara na madaraja mbalimbali
yanayounganisha jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake pia
imeharibiwa.
Picha ya anga ya mafuriko jijini Dar es Salaam, Tanzania
Mradi mwingine muhimu wa mabasi yaendayo kasi,
DART unaolenga kutatua tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam, nao
umeathiriwa na mafuriko hayo ambapo magari, mashine na mifuko ya saruji
imechukuliwa na maji hivyo kusitisha shughuli zake za ujenzi zilizo
katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo.
Shughuli za urejeshaji wa miundombinu zimekuwa
zikiendelea ikiwa ni pamoja na matengenezo katika daraja la Mpiji
linaloiunganisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Hata hivyo Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa
Tanzania, TMA, yametahadharisha kuhusu kuendelea kunyesha kwa mvua na
kuwataka watu wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhama ili kusalimisha
maisha na mali yao.
0 comments:
Post a Comment