Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa ni utovu wa nidhamu na ukosefu wa adabu kuwa baadhi ya
Watanzania kuwatukana, kuwadhihaki na kuwakejeli Waanzilishi wa Taifa la
Tanzania, Hayati Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amaan Karume.
Aidha, Rais
Kikwete amesema kuwa viongozi hao wawili wameifanyia Tanzania mambo
mengi, mambo makubwa na mambo ya kihistoria kiasi cha kwamba Watanzania
wanao wajibu wa kudumisha na kuenzi heshima yao kwa namna ya kudumu.
Akizungumza
na Wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari usiku wa jana, Jumatano,
Aprili 16 katika mahojiano maalum ya kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano,
Rais Kikwete amesema: “Ni kukosa adabu na ni utovu mkubwa wa
nidhamu kwa Mtanzania yoyote kuwatukana, kuwadhihaki ama kuwakejeli
waasisi wa Taifa letu. Hawa ni watu ambao waliifanyia nchi yetu mambo
makubwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mzee
Karume yule aliongoza Mapinduzi yaliyoondoa dhuluma na uonevu pale
Visiwani. Waafrika walio wengi walikuwa wanaonewa sana pale Tanzania
Visiwani, pengine watu wamesahau, lakini hata pale walipokuwa wanashinda
uchaguzi bado walikuwa hawapewi nafasi ya kuongoza maisha yao wenyewe.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Ni
ukosefu wa adabu kwa yoyote kumshutumu mtu aliyejitolea kiasi hicho ili
kubadilisha mfumo dhalimu na kujenga maisha na mazingira ya maisha bora
kwa wengi.”
“Mzee
Nyerere yule ametuachia Taifa moja, lililoungana, lenye umoja, lenye
amani na mshikamano. Misingi ambayo aliijenga yeye ndiyo imeendelea
kuongoza Taifa letu kwa miaka yote hii. Viongozi wengine wote ambao
wamemfuata yeye – Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na sasa mimi mwenyewe,
tumefuata na kuongozwa na misingi hii. Na siku nchi yetu inaamua
kuipuuza misingi hiyo, tutaingia katika matatizo makubwa.”
Rais
Kikwete ametoa msimamo huo baada ya kuwa ameulizwa kuhusu matusi,
kejeli, dhihaki ambazo zimekuwa zinaonyeshwa na wajumbe wachache wa
Bunge Maalum la Katiba juu ya waasisi hao wa Tanzania na Wabunifu Wakuu
wa Muungano wa Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Aprili, 2014
0 comments:
Post a Comment