WAANDISHI wa habari wametakiwa kuifahamu rasimu ya pili ya Katiba ili wasiipotoshe jamii wakati wa kupiga kura ya maoni.
Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya
masuala ya usalama kwa waandishi wa habari.
Alisema katika mchakato huo kila kinachoandikwa kwenye vyombo vya
habari wananchi wanaamini hivyo bila waandishi kuielewa vizuri rasimu
jamii itapotoshwa.
“Jamani waandishi wenzangu tuisome vizuri rasimu hii na yale
yanayopiganiwa katika Katiba… sisi ndio tutakuwa wa kwanza kulaumiwa
pindi wananchi watakapokuja kufanya uamuzi mbaya.
“Kumbukeni Katiba ni maisha ya miaka 50 ijayo hivyo kwa kuwapotosha
tutaipeleka nchi pabaya… ni muhimu tukasoma na kuelewa historia ya nchi
hasa Muungano kabla ya kuandika na kutangaza kwenye vyombo vyetu,”
alisema Kibanda.
Kwa mujibu wa Kibanda, wakati suala la muungano likiteka majadiliano
ya katiba kwa sasa, suala hilo lilikuwepo siku nyingi hata waasisi wa
muungano walilijua hilo.
Alisema kutoka na elimu ndogo iliyokuwepo awali, hata leo
wanaopigania serikali tatu au mbili hawajui matatizo gani yapo kwenye
muundo wanaoutaka, hawajui itawasaidia nini na kusisitiza kwamba
waandishi ni bora warudi kwenye historia ya muungano ili kutoa elimu
sahihi kwa jamii.
Kibanda alitumia fursa hiyo kumshauri rais atenge miaka mitano kwa
ajili ya kueneza elimu ya Katiba kabla ya kuanza mchakato wa kupata
Katiba mpya.
Kuhusu usalama wa waandishi wa habari, Kibanda alisema wanataaluma
hao ni miongoni mwa makundi yanayosakawa huku akibainisha kwamba kauli
tata zinazotolewa dhidi yao hasa na viongozi wa juu zinawafanya
wanataaluma hao kudharaulika machoni mwa watu na kujengewa chuki katika
jamii.
Miongoni mwa waandishi waliohudhuria semina hiyo ni Marine Hassan
Marin, aliyesema suala la usalama kwa waandishi ni muhimu kutolewa mara
kwa mara hata katika ofisi zao.
Kwa kipindi chote cha siku tatu walichokaa katika semina hiyo, Marin
alisema amejifunza mambo mbalimbali kuhusu kujilinda wakati wa kutafuta
habari ambayo awali alikuwa hayajui.
Na Nasra Abdallah
0 comments:
Post a Comment