Siku moja baada ya wabunge kuwataka Waziri
Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki kujiuzulu
kwa kushindwa kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili, meno 706 ya tembo
yamekamatwa jijini Dar es Salaam.
Meno hayo 706 ni sawa na tembo
353 waliouawa katika hifadhi za wanyama pori
mbalimbali hapa nchini. Tukio hilo
lililotokea jana jioni katika Mtaa wa Kifaru, Mikocheni, wilayani Kinondoni,
liliongozwa na Waziri Kagasheki ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Tarish Maimuna.
Waliokamatwa na shehena
hiyo ya meno ya tembo ni raia watatu wa China ambao ni Xu Fujie, Chen
Jinzha na Huang Qin wote kutoka mji wa Guandung .
Raia hao wa China wamekuwa wakiishi katika nyumba hiyo kwa
miaka mingi wakifanya biashara ya kuingiza nchini vitunguu swaumu kutoka China na
kusafirisha nje ya nchi makombe yanayopatikana baharini.
Alipoingia ndani ya nyumba
hiyo, Kagasheki ambaye aliambatana na askari polisi na baadhi ya maofisa
usalama alishuhudia shehena kubwa ya meno ya tembo ikiwa imehifadhiwa kwenye
viroba vyenye uzito wa kilo 50.
Mbali ya kushuhudia shehena
ya meno hayo, alionyeshwa gari maalumu aina ya Toyota Noah ambalo watuhumiwa
hao hulitumia kutoa pembe porini na kuyaingiza jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika eneo la
tukio mara baada ya kuwakamata alisema kukamatwa kwa watu hao kunatokana na
matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo imesitishwa na Serikali juzi
baada ya wabunge kuilalamikia.
Waziri Kagasheki alisema
kwamba katika harakati za kutaka kuwakamata watuhumiwa hao walitoa Sh30 milioni
kwa ajili ya kujaribu kuwahonga askari.
“Walitaka kuwahonga askari
ili wasikamatwe,” alisema huku akionyesha noti za fedha hizo.
Alisema wabunge wanaomtaka
ajiuzulu kwa madai kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili imesababisha mauaji ya
watu na mifugo wanapoteza muda kwa kuwa mwenye mamlaka ya kumtoa ni Rais Jakaya
Kikwete pekee.
“Sasa mimi nasema kunitoa
haitakuwa rahisi anayeweza kunitoa ni yule aliyeniweka,” alisema.
Alisema ipo mikakati
inayofanywa na baadhi ya wabunge kutaka kuwang’oa baadhi ya mawaziri kwa
masilahi binafsi ya kisiasa.
“Itakuwa ni jambo la ajabu
kwamba kila mtu akiingia madarakani wanataka atoke, watatolewa wangapi?”
alihoji na kuongeza kuwa operesheni hiyo ni muhimu kwa ajili ya kunusuru tembo
wasiishe.
Alisema kwamba ni kweli
kuna baadhi ya dosari zimejitokeza kwenye operesheni ikiwamo kuuawa kwa baadhi
ya mifugo, lakini siyo kwamba zoezi zima halina manufaa.
Kagasheki alisema kama kasi hii ya kuuawa kwa tembo itaachiwa iendelee
baada ya miaka 10 tembo wote watakuwa wameisha nchini.
Alisema hataki kuona
utawala wa Rais Kikwete ukiondoka madarakani ukiwa na lawama ya kuachia
majangili wawamalize tembo.
Mmoja wa watuhumiwa hao,
Huang Qin alisema shehena yote ya meno ya tembo iliyokamatwa nyumbani kwake
ilikuwa ikiletwa kidogo kidogo na rafiki yake ambaye hakumtaja jina.
Akiongea kwa Kiswahili Qin
alisema: “Mimi hii si yangu, kichwa yangu mbovu. Rafiki yangu alileta hii
(meno) kidogo kidogo.”
Januari mwaka huu, Gazeti
La Daily Mail la Uingereza liliripoti kwamba Serikali ya Kenya imekamata
shehena ya vipande 638 vya meno ya tembo ambavyo ni sawa tembo 320 waliouawa.
Mzigo huo wa tani mbili
ulikuwa kwenye kontena la mawe ya urembo (marumaru) kutoka Tanzania.
Taarifa zaidi zinaonyesha
kuwa tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya Dola za Marekani 3.4 milioni
sawa na takriban Sh5.4 bilioni zilikamatwa Hong Kong Oktoba 20, mwaka jana,
huku ikielezwa kuwa meno hayo yalikamatwa yakisafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.
Agosti 16 mwaka huu polisi
wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam, walimkamata raia wa Vietnam
akiwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh18.4 milioni yaliyotengenezwa kama bangili tayari kusafirisha kwenda nje ya nchi.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment