Mawaziri
wa Mambo ya Nje wa Nchi 9 zinazounda Kikosi Kazi cha Jumuiya ya Madola
chini ya Uenyekiti wa Tanzania wakishiriki kwenye Mazungumzo na
waandishi wa Habari baada ya kumaliza kikao chake cha 43 jijini London
Uingereza.
Mhe.
Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa
Tanzania akiwa kwenye kikao na Mabalozi wa Nchi za Afrika Wanachama wa
Jumuiya ya Madola jijini London, pembezoni mwa kikao cha Mawaziri wa
Kikosi Kazi cha Jumuiya hiyo.
Balozi
wa Tanzania nchini Uingereza Mhe. Peter Kallaghe akimkaribisha Mhe.
Bernard Membe, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Nchi za Jumuiya
ya Madola kuzungumza na Mabalozi wa Nchi za Kiafrika wanachama wa
Jumuiya hiyo.
Mhe.
Benard Membe, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Jumuiya ya
Madola akimkaribisha Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo Mhe.
Kamalesh Sharma alipofanya naye mazungumzo kabla ya Mkutano wa 43 wa
Kikosi Kazi hicho kuanza.
Mhe. Bernard Membe (Mb.),
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ametoa wito kwa Nchi
za Kiafrika Wanachama wa Jumuiya ya Madola kuunganisha nguvu na kuwa na
sauti moja itakayotetea maslahi ya nchi za kiafrika kwenye jumuiya
hiyo.
Mhe. Membe aliyasema hayo
alipokutana na Mabalozi wa Nchi 12 za Kiafrika wanaowakilisha nchi zao
kwenye Jumuiya ya Madola pembezoni mwa Mkutano wa Kikosi Kazi cha
Mawaziri cha jumuiya hiyo kilichofanyika Jijini London Uingereza tarehe
13-14 Machi 2014.
Kwenye mazungumzo yao Mhe.
Membe aliwakumbusha Mabalozi hao chimbuko la jumuiya hiyo na ushiriki wa
nchi za kiafrika ili kutetea maslahi ya Waafrika na hatimaye kuvuna
matunda ya ushiriki wa Waafrika kwenye Jumuiya ya Madola.
“Kama wanachama kutoka Bara la
Afrika, ni wajibu wetu kushikamana na hata pale mwanachama mmoja
anapotolewa au anapowekewa vikwazo vya ushiriki, tuungane na kuhakikisha
mwanachama huyo anaondolewa vikwazo na hatimaye kurudi kwenye jumuiya.
Tusipofanya hivyo hata sisi tutakuwa na tatizo” alisema Mhe. Membe.
Aliwaasa kuwa na sauti moja
katika kutetea haki za ushiriki wa nchi za Kiafrika ndani ya jumuiya
hiyo. Alisema namba ya nchi za Afrika kwenye jumuiya hiyo ni kubwa na
hivyo ushiriki wa Waafrika lazima uwe wa kushindo.
Alisisitiza kuwa na sauti moja
ya Waafrika kutakemea masuala yanayokuja kama shinikizo kutoka wanachama
wa Nchi za Magharibi kama vile ndoa za jinsia moja, ambayo yanagusa
dini, tamaduni, mila na desturi za Kiafrika. Alisema upepo wa shinikizo
hilo unavuma kwa kasi kana kwamba kukubaliana na masuala hayo kutaondoa
umaskini barani Afrika. Nchi za Kiafrika kwenye Jumuiya hiyo zina wajibu
wa kushiriki kikamilifu kwa kusimamia agenda zitakazoleta maendeleo
barani Afrika.
Ili kufanikisha wajibu huo,
Mhe. Membe aliwahimiza Mabalozi hao kushiriki kwenye chaguzi mbalimbali
za jumuiya, kutoa taarifa kwa Wakuu wa Nchi na Serikali zao kutoka
Makao Makuu ya Sekretarieti ya Jumuiya hiyo yaliyopo London Uingereza na
mwisho kuhakikisha wanashiriki kikamilifu na kutoa sauti ya pamoja
kwenye shuguli mbalimbali za Jumuiya badala ya kusubiri wengine wafanye
maamuzi kwa niaba yao.
Kwa upande wao, mabalozi hao
walimpongeza Mhe. Membe kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kikosi Kazi
cha Mawaziri cha jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka miwili. Aidha
walisifu jitihada za Tanzania kutetea maslahi ya nchi za Kiafrika
wanachama wa jumuiya hiyo.
Kwa upande mwingine
walilalamikia uongozi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kwa
kutoshirikiana na mabalozi hao hususan kwenye maandalizi ya Vikao vya
Wakuu wa Nchi na Serikali wanachama au baada ya vikao hivyo. Waliongeza
kuwa kero za kiutendaji zinafanyiwa kazi juu juu tu na badala yake
zinazua kero kubwa zaidi. Hivyo walimuomba Mhe. Membe kuwasaidia kwa
kupitia Vikao vya Kikosi Kazi cha Mawaziri kuondoa changamoto hizo.
Ndani ya Jumuiya ya Madola kuna
nchi za Kiafrika 18 ambapo 12 kati ya hizo zilizoshiriki kwenye mkutano
huo ni; Mauritius, Cameroon, Seychelles, Namibia, South Africa, Uganda,
Kenya, Mozambique, Ghana, Lesotho, Zambia na Tanzania. Jumuiya ya
Madola ina jumla ya nchi 53.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

0 comments:
Post a Comment