Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akizindua nembo wakati wa uzinduzi rasmi
Umoja wa vikundi vya Wanawake Mbagala (UWAMBA) katika sherehe
iliyofanyika kwenye ukumbi wa Dar Live.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akiongea wakati wa uzinduzi rasmi Umoja wa
vikundi vya Wanawake Mbagala (UWAMBA) katika sherehe iliyofanyika kwenye
ukumbi wa Dar Live.
Na Anna Nkinda – Maelezo
Wanawake
wajasiriamali nchini wametakiwa kutengeneza bidhaa ambazo zinahitajika
kwa wingi na watumiaji na kuacha kung’ang’ania kutengeneza bidhaa
ambazo soko lake ni dogo.
Mwito
huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)
Mama Salma Kikwete wakati wa uzinduzi wa umoja wa vikundi vya kuweka na
kukopa Mbagala (UWAMBA) vilivyo chini ya WAMA uliofanyika katika Ukumbi
wa Dar Live jijini Dar es Salaam.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema
changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wengi ni upatikanaji wa
soko la bidhaa zao lakini kama wataamua kubadilika na kutengeneza bidhaa
ambazo zinahitajika kutapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.
“Ni
jambo jema kujifunza kutengeneza bidhaa mbalimbali , lakini kama utaona
bidhaa uliyojifunza haina soko unaweza kutengeneza bidhaa nyingine
ambayo watu wengi wanaihitaji jambo la muhimu ni kuwa makini katika
umaliziaji wa kutengeneza bidhaa nzuri na zinazovutia”, alisema Mama
Kikwete.
Akizungumzia
kuhusu umuhimu wa vikundi hivyo kwa jamii Mwenyekiti huyo wa WAMA
alisema vikundi hivyo vinatoa mafunzo ya kuweka akiba na kukopa kwa
namna ambayo inamsaidia mwanakikundi kujenga tabia ya kujichunga katika
matumizi ya pesa na hivyo kuwa na mawazo ya kuweka akiba mara kwa mara.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akikata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi
rasmi Umoja wa vikundi vya Wanawake Mbagala (UWAMBA) katika sherehe
iliyofanyika kwenye ukumbi wa Dar Live.
Aidha
Mama Kikwete pia aliwataka wanawake hao kujitokeza kwa wingi kugombea
na kushiriki katika chaguzi mbalimbali zinazokuja ili wapate nafasi ya
kutoa maamuzi.
Mwenyekiti
wa WAMA alisema , “Mkipendana, kushirikiana na kusaidiana mtafika
mbali, ondoeni tofauti zenu na kila mmoja asimame na kuweza kumtetea
mwenzake, muwe na marafiki wanaopenda maendeleo na kama mwenzako
akifanya vizuri usiache kumsifia”.
Akisoma
risala ya UWAMBA Halima Abrahman ambaye ni katibu wa kikundi cha Faraja
kilichopo Tandika alisema umoja huo wenye vikundi 11 huku wanachama
wake wengi wakiwa ni wanawake na wachache ni wanaume ulianzishwa mwaka
2013 wakiwa wanachangia hisa moja kwa shilingi 2000 kwa sasa wana akiba
ya zaidi ya shilingi milioni 15.
“Mbali
na hisa mapato ya kikundi chetu yanapatikana kutokana na wanachama
kufanya biashara mbalimbali zikiwemo za utengenezaji wa sabuni za maji,
batiki, mishumaa, vikapu, mifuko ya karatasi, siagi za karanga, kusuka
mikeka, unga wa muhogo na achali”, Halima alisema.
Alizitaja
changamoto zinazokikabili kikundi hicho kuwa ni pamoja na ufinyu wa
bajeti, ukosefu wa ofisi na vifaa vya kuhifadhi taarifa za chama,
kushindwa kushiriki katika mafunzo na ukosefu wa masoko ya bidhaa zao.
Ili
kukabiliana na changomoto zinavyovikabili vikundi hivyo Mama Kikwete
aliwakabidhi vyerehani vinne ambavyo vitatumika kuanzisha mradi wa
kushona nguo ambao utawaongezea kipato na Kompyuta moja kwa ajili ya
kuweka kumbukumbu zao.
Mwenyekiti
wa WAMA na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisaidiana na Mama Tabu
Likoko kutoka WAMA, wakimkabidhi Mwenyekiti wa UWAMBA, Mama Zenna Hanga
moja ya charahani walizozitoa kwa umoja huo wakati wa sherehe za
uzinduzi huko Mbagala.
Vikundi
vinavyosimamiwa na Taasisi ya WAMA vimetokana mradi wa majaribio wa
MWANAMKE MWEZESHE ambao ulianza mwaka 2011 uliolenga kuanzisha mfumo wa
vikundi ambavyo vitaweza kutoa fursa za mikopo, mafunzo na kujenga
uwezo wa wanachama kujiendesha wenyewe na kuanzisha miradi ambayo
itawaongezea kipato.
Mradi
huo wa majaribio ulifanikiwa na kuweza kuwafikia watu zaidi ya 1200 kwa
kata zilizopo katika maeneo ya Majohe, Gongo la Mboto, Mbagala ,
Manzese, Temeke na Tandika. Ambapo jumla ya akiba ya zaidi ya milioni
200 zimekusanywa na mikopo ya shilingi milioni 265 imeweza kufikia
vikundi mwaka 2013
Pia
mradi huo umeweza kuunganisha vikundi na kuvipatia fursa za kiuchumi na
kijamii kwa kutoa mafunzo na semina mbalimbali za wanavikundi ikiwa ni
pamoja na mafunzo ya usindikaji, kuwaunganisha na huduma ya bima ya afya
na ushiriki wa maonyesho ya biashara kwa ajili ya kutangaza bidhaa zao.
Wanachama
wa UWAMBA wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi Mama Salma
Kikwete wakati wa sherehe ya uzinduzi wa umoja wao huko Dar Live
Mbagala.
Mwenyekiti
wa WAMA na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete akiangalia bidhaa mbalimbali
zinazozalishwa na wana UWAMBA wakati wa sherehe za uzinduzi wa kikundi
cha huko Mbagala.(Picha na John Lukuwi).
CHANZO:MO BLOG
0 comments:
Post a Comment