Mwalimu
wa Shule ya Msingi Misunkumilo, Kata ya Namanyere, wilayani Nkasi,
mkoani Rukwa, Oswald Kapota (33) amehukumiwa kwenda jela miezi sita kwa
kosa la kutelekeza familia yake na kwenda kuishi kwa kimada.
Mwalimu
huyo ambaye ameshindwa kubaki njia kuu na kuendeleza michepuko, amepata
hukumu hiyo juzi baada ya Mahakama ya Mwanzo Namanyere, kumtia hatiani.
Akitoa
hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Namanyere, Baraka Stanley,
alisema kuwa mahakama hiyo imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande
wa mashitaka ambao unaonyesha kuwa Mwalimu huyo alifanya kitendo hicho
kwa kukusudia.
Mwalimu
huyo alidaiwa kuitelekeza familia yake ya watoto wawili na mke, kisha
kuhamia nyumbani kwa mwanamke mwingine na kuifanya familia hiyo kuishi
katika mazingira magumu kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita, hali
iliyomlazimu mkewe kufungua kesi polisi ya kudai huduma ya malezi ya
familia hiyo.
Licha
ya hukumu hiyo mahakama imeamuru mwalimu huyo atakapomaliza adhabu yake
ya kifungo jela atalazimika kuitunza familia yake kama wajibu
unavyomtaka kama mzazi.
Awali
upande wa mashitaka uliieleza mahakama hiyo kuwa mwalimu huyo
alimtelekeza mke wake, Lucy Malambugi, ambaye amezaa naye watoto wawili
kiasi cha kuifanya iishi maisha magumu huku mkewe akihangaika kuomba
omba ilhali yeye akiponda raha na nyumba ndogo.
Kabla
ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mshitakiwa alitakiwa kujitetea ambapo
alikataa kutoa utetezi wake kwa madai kuwa hawezi kujitetea mbele ya
mwanamke huyo, akimtuhumu kuwa si mwaminifu kwenye ndoa na ndiyo chanzo
cha yeye kuamua kuhamia kwa nyumba ndogo.
Kutokana
na kosa hilo, mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa huyo chini ya kifungu
cha sheria namba 167, sura ya 16, ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka
2002.
CHANZO:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment