Habari
kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa askari hao waliokuwa wamevalia kiraia,
walifanya uvamizi huo majira ya saa 11:00 jioni, kwa kile kilichodaiwa
kuwa walikuwa wakiwatafuta watuhumiwa wa wizi wa pikipiki.
Baadhi
ya wakazi wa eneo hilo waliozungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti,
walisema katika tafrani hiyo, wananchi wawili raia wa Tanzania, ambao
majina yao hayajapatikana, walijeruhiwa kwa risasi.
Kwa mujibu wa habari hizo, kati ya majeruhi hao, mmoja anadaiwa kujeruhiwa kwenye kiganja na mwingine mguuni.
Habari hizo zinaeleza kuwa baada ya wananchi kuona wenzao wamejeruhiwa, walianza kupambana na askari hao.
Hali hiyo inadaiwa kusababisha baadhi ya askari hao kukimbia na kuvuka mpaka kuingia nchini kwao.
Hata
hivyo, imeelezwa kwamba mmoja kati ya askari hao w aUganda, alizingirwa
na wananchi ambao walikuwa tayari kujichukulia sheria mkononi.
Walisema
baada ya askari huyo kuhofia kuuawa na wananchi, alikimbia na
kujisalimisha katika Kituo cha Polisi kilichoko Mutukula upande wa
Tanzania ambapo alikamatwa na kuwekwa rumande.
Askari huyo ambaye jina lake halijafahamika hadi sasa, bado anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kagera kwa mahojiano zaidi.
Aidha, habari zaidi zilidai kuwa askari waliokimbia na kuingia Uganda waliwakamata raia wawili wa Tanzania na kuondoka nao.
Kwa mujibu wa habari hizo, ufuatiliaji wa kujua waliokamatwa na kuchukuliwa na askari hao ni akina nani unaendelea.
Hata
hivyo, wananchi wanaoishi Mutukula walidai kuwa siyo mara ya kwanza
askari kutoka Uganda kuvamia eneo hilo na kukamata Watanzania wanaoishi
mpakani na kuondoka nao bila kushirikisha polisi wa Tanzania.
“Huu
siyo utaratibu. Ni ubabe. Hata kama kuna Watanzania wanawahisi kuhusika
na uhalifu katika nchi yao, inabidi wafuate utaratibu kwa kutoa taarifa
ili askari wa Tanzania washiriki kuwatafuta wahalifu husika,” alisema
mwananchi mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa.
Kwa
mujibu wa wananchi hao, askari walioingia nchini na kufanya tukio hilo
ni askari polisi kutoka eneo la Mbarari nchini Uganda.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga, alipoulizwa na waandishi wa
habari ofisini kwake kuhusiana na tukio hilo, alithibitisha, lakini
akasema yeye hana mamlaka ya kulizungumzia zaidi mpaka apate ruhusa
kutoka Makao Makuu ya Polisi.
“Hili
ni suala la kiusalama linalohusisha nchi na nchi, siwezi kulizungumzia
zaidi, tunachokifanya kama kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa tunaandaa
taarifa tuitume polisi makao makuu, wenyewe ndiyo wataamua kama ni
kuniruhusu mimi nizungumze au wazungumze wao makao makuu,” alisema
Kamanda Mayunga.
Kamanda
huyo alisema kuwa kwa kawaida masuala yanayohusu nchi na nchi serikali
huwa inakuwa makini sana kuyazungumzia, hivyo subira inahitajika ili
watoe taarifa iliyo sahihi.
Msemaji
wa Jeshi la Polisi Makao Makuu jijini Dar es Salaam, Advera Senso,
alipoulizwa na NIPASHE jana, alisema kinachopfanywa na jeshi hilo kwa
sasa ni kuchunguza kujua ilikuwaje askari hao watoke Uganda na kuingia
Tanzania bila kuwaarifu polisi wenzao wa Tanzania.
“Tunahitaji
kufanya hivyo ili kila nchi ijiridhishe. Hilo ndilo suala la msingi
ki-nchi na kisera. Na hiyo ndiyo maana ya kuwapo Interpol (Polisi wa
Kimataifa). Tuna ushirikiano,” alisema Senso.
Hata hivyo, alisema baada ya undani wa suala hilo kujulikana, taarifa zitatolewa na jeshi hilo ngazi ya mkoa (Kagera).
0 comments:
Post a Comment