Kificho jana alikana maoni hayo ya kutaka serikali tatu na kwamba
kilichoelezwa na Jaji Warioba siyo tafsiri sahihi ya mapendekezo yao
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kutoka Chama cha
Mapinduzi (CCM) juzi jioni walipata wakati mgumu katika kikao cha ndani
cha wabunge wa chama hicho wakituhumiwa kwa ‘usaliti wa Muungano’.
Kilichowaponza wajumbe hao ni kupitisha mabadiliko
ya Katiba mwaka 2010 yanayoitaja Zanzibar kuwa ni nchi na hivyo kuvunja
Katiba ya Muungano na kitendo cha baraza hilo kupendekeza Serikali tatu
mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kikao hicho kilifanyika muda mfupi baada ya Jaji
Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba akieleza kuwa changamoto
kubwa za Serikali mbili ni uvunjaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano,
uliotokana na Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Katika hotuba yake, Jaji Warioba alisema pia kuwa
baraza hilo lilipendekeza mfumo wa Serikali tatu kutokana na maelezo
kuwa linataka Zanzibar huru, Tanganyika huru na Serikali ya Muungano
huru na kila chombo kuwa na mamlaka yanayotambuliwa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichoongozwa
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, zinaeleza kuwa wabunge wa CCM hasa wa
Bara walielekeza lawama kwa viongozi wa Zanzibar hasa Baraza la
Wawakilishi kutokana na kuwasaliti.
Chanzo chetu kimemtaja mmoja wa wazungumzaji,
Christopher Ole Sendeka kwamba alieleza kwa uchungu kuwa mabadiliko
yaliyofanywa na Zanzibar ni usaliti mkubwa kwa Serikali ya Muungano.
“Sendeka aliongea kwa uchungu kuhusu Zanzibar
kuvunja Katiba ya Muungano na alisema lazima chama kichukue hatua ili
kunusuru Muungano,” alisema mjumbe mmoja wa kikao hicho.
Alipoulizwa kuhusu kauli hizo, Sendeka hakukanusha
wala kukubali, bali alisema hayo ni masuala ya kikao cha ndani na
hawezi kuyazungumzia.
Mbunge mwingine aliyetajwa kuzungumza ni
Silivester Mabumba wa Jimbo la Dole, ambaye alieleza wazi kuwa ni vyema
kuacha unafiki kuwa mnataka Serikali mbili wakati kuna mabadiliko ambayo
mmepitisha kuwa Zanzibar ni nchi. Hata hivyo, Spika wa Bunge la Baraza
la Wawakilishi, Pandu Amir Kificho baada ya kushambuliwa alieleza
kutofautiana na kile ambacho kimeelezwa katika hotuba ya Jaji Warioba.
Kificho, licha ya kukiri kuwa mmoja wa waliosaini
taarifa ya baraza hilo, alisema bado msimamo wa baraza ulikuwa ni
Serikali mbili. Kauli hiyo ilithibitishwa jana baada ya kufafanua katika
kituo kimoja cha televisheni kuwa msimamo wa baraza haujawahi kuwa ni
Serikali tatu.
Baada ya lawama nyingi, inadaiwa wajumbe hao,
walifikia azimio la kuandaa utaratibu wa kufanyia mabadiliko ya Katiba
ya Zanzibar kupitia kura ya maoni.
“Tumewaambia waone uwezekano wa kuifanyia
marekebisho Katiba yao kama ukipitishwa muundo wa Serikali mbili,”
alisema mjumbe mmoja.
CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment